Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz Ki utapigaje pale, Diarra utadakaje?

Stephane Aziz KI VS Diarra Aziz Ki utapigaje pale, Diarra utadakaje?

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hatua ya makundi ya michuano ya Afcon 2023, ilitamatika Jumatano usiku, wiki hii na sasa imefungua njia kwa hatua muhimu ya 16 Bora.

Hatua ya makundi ilikuwa na mshangao kwenye kila mchezo huku ikishuhudiwa baadhi ya mataifa makubwa kwenye soka yakitupwa nje ya michuano hiyo.

Leo tunaingia kwenye hatua nyingine ambapo kila kigogo anakutana na mwenzake na lazima mataifa manane tu yapenye kwenye hatua inayofuata, yaani robo fainali.

Hata hivyo, kwa mashabiki wa soka hapa nchini wameanza kutania kuhusiana na mechi inayowakutanisha nyota wa Yanga wanaoziwakilisha nchi zao, yaani Stephen Aziz KI wa Burkina Faso na Djigui Diarra anayeichezea Mali ambayo itapigwa keshokutwa Jumatatu, utani uliopo mitaani kwa sasa unashahirishwa na maneno flani ya kitaani eti "umepigaje hapo Aziz Ki na Umedakaje pale Diarra".

Mali v Burkina Faso

Burkina Faso ilimaliza hatua ya makundi kwa majonzi baada ya kuchapwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Angola.

Wabishi Mali walimaliza michezo ya hatua ya makundi bila kupoteza mchezo wowote. Presha hapa siyo mechi hiyo, bali ni mashabiki nchini kugawanyika kutokana na nchi hizo kuwa na wachezaji wawili ambao wanacheza Ligi Kuu Bara wakiwa na Yanga, Aziz Ki wa Burkina Faso na Diarra akiwa na Mali.

Mali ina rekodi ya kushika nafasi ya tatu kwenye Afcon mara mbili, 2012 na 2013, huku Burkina Faso ikiwa na rekodi ya kumaliza nafasi ya pili 2013. Uwanja: Mechi hii inapigwa Amadou Gon Coulibaly, Jumatatu kuanzia saa: 2:00 usiku.

Kipa wa Mali, Djigui Diarra

Nigeria v Cameroon

Pamoja na kuanza vibaya, wababe hao wa soka la Afrika walifanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora baada ya michezo yao ya mwisho ya kundi.

Nigeria inakwenda kwenye mchezo huu ikitaka kumaliza kipindi cha miaka 10 cha ukame wa Kombe la Mataifa Afrika, lakini itakutana na Cameroon ambayo kocha wake Rigobert Song ameshasema kutakuwa na presha kubwa kwake kama hawatavuka hatua hii.

Song yupo kwenye wakati mgumu kutokana na timu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi, baada ya kushinda mchezo mmoja tu kati ya mitatu ya hatua hiyo.

Makombe: Cameroon imeshatwaa ubingwa wa Afcon mara 5, Nigeria imechukua mara 3. Uwanja: Mechi hii inapigwa leo kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny saa: 5:00 usiku

Cape Verde v Mauritania

Baada ya kuishangaza dunia kwa kufuzu hatua ya 16 Bora bila kupoteza mchezo pamoja na kwamba walipangwa na vigogo Misri na Ghana, Cape Verde wanakwenda kukutana na wabishi wengine Mauritania.

Hizi ni timu mbili ambazo zilikuwa hazipewi nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya 16 bora, lakini zimepenya kibabe na sasa zinakutana keshokutwa.

Nchi hizi zote zinatajwa kuwa changa kwenye historia ya soka la Afrika, zikiwa hazijawahi kutwaa ubingwa huu.

Mafanikio makubwa ya Cape Verde kwenye michuano hii ni kufika robo fainali mwaka 2013, kwa Maurtania ambayo imeshiriki michuano hii mara mbili, iliishia hatua ya makundi mwaka 2021.

Uwanja: Mechi hii inapigwa keshokutwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny saa: 2:00 usiku.

Equatorial Guinea v Guinea

Timu nyingine ambazo zimewashangaza wengi kwenye michuano hii ni Equatorial Guinea, ambayo ilimaliza kinara kundi lake ambalo lilikuwa na vigogo Ivory Coast na Nigeria, itavaana na Guinea ambayo imefuzu pamoja na kuwa na matokeo ya kushangaza.

Guinea ambayo ilifuzu ikiwa na pointi nne, itakuwa na wakati mgumu wa kuvaana na Equatorial ambayo staa wake Emilio Nsue, amefanya mambo makubwa na sasa ndiye kinara wa mabao kwenye michuano hii akitupia nyavuni mara tano.

Hizi ni timu nyingine ambazo hazina rekodi kubwa kwenye michuano hii, huku Equatorial ikiwa na rekodi ya kuishia nafasi ya nne mara moja, mwaka 2015 na Guinea ikiwa hii ndiyo mara yao ya kwanza kushiriki.

Uwanja: Mechi hii inapigwa kesho kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara saa 2:00 usiku.

Angola v Namibia

Namibia imeweka rekodi ya kufuzu hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza kuanzia ilipoanza kushiriki mwaka 1998. Raundi hii inakwenda kuvaana na Angola ambayo imefanya makubwa kwenye hatua ya makundi ikiwa ni kati ya timu chache ambazo hazijapoteza mchezo kwenye hatua hiyo.

Angola ambayo imefika robo fainali mara mbili 2008 na 2010, inataka kuendeleza rekodi ya nchi hiyo kwenye michuano hii mikubwa Afrika.

Namibia haijawahi kuvuka hatua ya makundi, hii ni mara yao ya kwanza. Uwanja: Mechi hii inapigwa leo kwenye Uwanja wa Bouake saa 2:00 usiku.

Misri vs D.R Congo

Misri imefuzu hatua hii kibishi baada ya kutoka sare kwenye michezo yote mitatu ya makundi.

Hili halikuwa jambo linatarajiwa na wengi kutokana na rekodi zao kwenye michuano hii kuwa ndiyo timu yenye mafanikio makubwa zaidi.

Inakwenda kuvaana na DR Congo ambayo imeonyesha kiwango kizuri na kufuzu hatua ya 16-Bora ikishika nafasi ya pili kundi F, lakini ikionekana kupania vilivyo fainali za mwaka huu.

Huu ni mchezo mwingine ambao mashabiki wa soka la Tanzania wanausubiri kwa kuwa yupo beki wa Simba, Henock Inonga, akiwa ameshacheza michezo miwili kati ya mitatu ya nchi yake kwenye fainali hizi.

Misri ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hii mikubwa zaidi Afrika wakitwaa taji la Afcon mara saba, huku DR Congo ikiwa imelibeba mara mbili. Mechi hii inapigwa kesho kwenye Uwanja wa Laurent Pokou, kuanzia saa 5:00 usiku.

Senegal vs Ivory Coast

Ivory Coast ilishakata tamaa ya kufika kwenye hatua hii baada ya kudhalilishwa kwa kichapo kikubwa zaidi kwao kihistoria cha mabao 4-0 kutoka kwa Equatarial Guinea lakini matokeo ya Zambia na Morocco yakawapeleka 16-Bora, sasa inakwenda kuvaana na mabingwa watetezi Senegal.

Senegal iko katika ubora wake. Imefanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya Afcon ikiwa imemaliza na ushindi wa asilimia 100 kwa mara ya kwanza katika historia yake, huku Ivory Coast ikiwa imeshinda mchezo mmoja tu na kupoteza miwili. Ivory Coast ni kati ya timu kubwa kwenye michuano hii ikiwa imetwaa ubingwa mara mbili na Senegal mara moja.

Uwanja: Mechi hii inapigwa kwenye Uwanja wa Charles Konan Banny, Jumatatu saa 5:00.

Morocco vs Afrika Kusini

Rekodi ya Morocco ya kufika nusu fainali kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizopita bado haijawabeba kwenye michuano hii msimu huu.

Sasa inakwenda kuvaana na timu yenye uchu wa mafanikio, Afrika Kusini kwenye mchezo mwingine unaosubiriwa kwa hamu kubwa.

Morocco ina sare moja kwenye michezo mitatu ya makundi, huku Afrika Kusini ikikusanya pointi nne kwenye michezo mitatu.

Afrika Kusini imetwaa ubingwa wa Afcon mara moja, Morocco nayo ikichukua mara moja.

Uwanja: Mechi hii inapigwa kwenye Uwanja wa Laurent Pokou, Jumanne saa 5:00 usiku.

Chanzo: Mwanaspoti