Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz Ki habari nyingingine, Kibwana amtega Djuma

Azizi Ki Stephen 2 Aziz Ki habari nyingingine, Kibwana amtega Djuma

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kama usajili ambao mabosi wa Yanga wanaweza kujivunia, basi ni ule wa mshambuliaji Stephen Aziz Ki kwani amezidi kuwa na umuhimu kwenye kikosi.

Ki wakati anasajiliwa alitikisa, lakini wapo walioona hataisaidia Yanga baada ya kutoanza vizuri lakini sasa ameanza kuwaka.

Kwenye mchezo wa juzi Jumanne mshambuliaji huyo alitoa pasi mbili za mabao kati ya matatu waliyoshinda dhidi ya Coastal Union wakishinda mabao 3-0.

KI HABARI NYINGINE

Licha ya straika Fiston Mayele kuwa kinara wa mabao akifunga 13, uwepo wa Aziz Ki ndani ya Yanga unamfanya azidi kuwa tishio.

Ki ana uwezo wa kukaa na mpira miguuni huku akilazimisha mashambulizi langoni mwa timu pinzani na mara nyingi amekuwa akifanikiwa.

Kwenye mchezo huo, Ki alikuwa kwenye ubora hasa katika kukaa na mpira, sambamba na kusambaza kwa wenzake jambo ambalo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuwapa tabu wachezaji wa Coastal.

Mshambuliaji huyo alihusika kwenye mabao mawili huku pasi yake ya bao la pili alitoka na mpira golini kwao na kukimbia nao kisha alipiga pasi iliyokwenda moja kwa moja miguuni kwa Fiston Mayele aliyemchungulia kipa wa Coastal, Mahamud Mroivili na kuutupia wavuni.

MAYELE HAGUSIKI

Mayele kwenye mchezo huo alionyesha kuhitaji mabao kwani mara kwa mara alikuwa anapambana kwenye eneo la ushambuliaji ili atupie wavuni, na juzi aling’ara.

Mayele alitumia zaidi nguvu kuhakikisha anaipa presha safu ya ulinzi Coastal Union na alifunga bao la kwanza dakika ya 28 na dakika ya 66 alifunga la pili.

Mshambuliaji huyo aliwapa tabu mabeki wa Coastal akitumia spidi yake sambamba na nguvu hali iliyofanya washindwe kumdhibiti kwa urahisi

LOMALISA ANAWAKA TU

Joyce Lomalisa ndani ya Yanga ni beki anayezidi kuwa kwenye kiwango bora kadri siku zinavyozidi kwenda akianza kujihakikishia namba ya kucheza kwenye upande wa beki ya kushoto.

Lomalisa kwenye mchezo huo Yanga ilitumia zaidi upande wake kwenye kupeleka mashambulizi kwa wapinzani wao akicheza sambamba na Farid Mussa na walifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Beki huyo alitoa pasi ya bao la kwanza alilofunga Mayele na kumfanya afikishe idadi ya pasi za mabao nne akiwa ndiye kinara wa pasi za mabao kwenye kikosi cha Yanga kwa sasa.

VICENT, AMZA BASI TU

Upande wa Coastal Union eneo la ushambuliaji walicheza Vicent Abubakar na Moubarack Amza ambao walikuwa kwenye maelewano yasiyokuwa bora zaidi na muda mrefu walikuwa chini ya ulinzi.

Vicent alionekana kuwa mjanja alipokuwa akikabwa kwani alihama kutoka upande mmoja kwenda mwingine na alijaribu kupiga mashuti akiwa nje ya boksi.

Kwa upande wake, Amza alikuwa mtulivu akiwa chini ya ulinzi wa mabeki Yanick Bangala na Bakari Mwamnyeto, lakini alipambana alivyoweza ingawa alikosa msaada.

Mshambuliaji huyo alionyesha umahiri wa kukaa na mpira hata kama wachezaji wenzake wakikosekana kwenye eneo husika.

KIBWANA AMTEGA DJUMA

Beki wa kulia wa Yanga, Kibwana Shomari aliendelea kuwa kwenye ubora wake katika mechi hiyo huku Djuma Shaban ambaye anacheza namba hiyo akiwa benchi.

Kibwana aliweza kuwatuliza mawinga wa Coastal Union walioongozwa na Hamad Majimengi.

Kitendo cha kuwafanya mawinga hao wasicheze watakavyo kilimfanya asiende kupeleka mashambulizi kwa Coastal Union na Yanga ililazimika kutumia upande wa kushoto.

MAKOCHA WAFUNGUKA

Akizungumza baada ya mchezo, Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema ushindi walioupata kwenye mchezo huo ni sehemu ya morali kwa ajili ya mechi ijayo dhidi ya Azam.

“Huu ni ushindi mzuri kwa wachezaji wangu kwa sababu tuna mechi ngumu ijayo. Tumesahau haya matokeo na sasa tunaanza kujipanga kwa mechi inayokuja ambayo ni ngumu zaidi,” alisema Kaze.

Upande wa kocha msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro alisema walistahili kufungwa kutokana na wapinzani wao kuwa kwenye ubora wa hali ya juu.

“Tulitengeneza nafasi mara kadhaa lakini hatukuzitumia, wenzetu nafasi zao zote walizitumia vizuri, wametufunga kwa sababu walistahili.”

Chanzo: Mwanaspoti