Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz Ki apewa siku spesho Yanga, wanaoachwa wahaha mjini

Aziz Kiii Stephane Aziz Ki

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano na Usajili wa Yanga, Injinia Hersi Said amefichua kuna silaha mbili za kimataifa zinashuka kwa mpigo na ndiyo utakuwa mwisho wa usajili wa wageni kwa msimu ujao.

Lakini Mwanaspoti linajua kuna wachezaji watatu wamepewa mkono wa kwaheri. Wachezaji hao, Deus Kaseke, Balama Mapinduzi na Paul Godfrey ‘Boxer’ na Yacouba Sogne atatolewa kwa mkopo.

Juzi Jumanne, wachezaji waliitwa ofisi za mfadhili wa klabu hiyo (GSM) kwa lengo la kumalizana nao na kuwatakia maisha mema kwenye majukumu yao mapya nje ya Yanga.

Hersi alipoulizwa jana alisema; “Wapo wachezaji tunaowaacha, listi tutaitoa hivi karibuni, lakini kwa wageni tumebakiza wachezaji wawili ambao itakuwa ni sapraizi kwa mashabiki wetu.”

Mapema jana, mmoja wa vigogo wa Yanga aliliambia Mwanaspoti tayari klabu imewapa mkono wa kwaheri wachezaji hao ambao imeamua kuachana nao mapema kabla ya dirisha kufungwa ili waweze kuendelea na maisha mengine ya soka kwenye klabu nyingine na inaelezwa wachezaji hao wamekuwa wakipiga simu ili kupata timu zitakazowasajili msimu ujao na kuwahi dirisha la usajili kabla halijafungwa.

Hadi sasa Yanga imewatambulisha Bernard Morrison na Lazarous Kambole, huku ikitarajia kumtambulisha Aziz Ki Julai 9 baada ya uchaguzi mkuu, ingawa Hersi hakutaka kuliweka wazi hilo ili iwe sapraizi.

“Huenda ikawa hivyo au isiwe hivyo, tusubiri,” alisema Hersi huku akitabasamu na kusisitiza, wachezaji wa kigeni ambao imebakiza kwenye usajili wao ni wawili.

Alisema wamemtangaza mshambuliani Kambole, Morrison, kutakuwa na sapraizi ya wachezaji wengine wa kigeni ambao watatumia utaratibu kama uliofanywa kwa hao wengine kuwatambulisha.

Mwanaspoti linajua Kocha wa Yanga, Nabi Mohammed amewaambia viongozi wafanye kufuru yoyoye, winga Simon Msuva akiwashe na Fiston Mayele Jangwani msimu ujao hata kama ni kwa muda mfupi.

Mwanaspoti linajua Nabi alipagawa zaidi na Msuva na kuanza kufikiria fomesheni yao baada ya kuangalia mechi ya hisani ya timu Kiba na Samata.

Lakini habari za uhakika zinasema kwamba uwezekano huo ni mdogo kwani Msuva ameshikilia msimamo wake wa kwenda kucheza Uturuki ingawa nako inaelezwa nafasi ni finyu kwavile amekaa nje ya uwanja muda mrefu.

Yanga ilitaka kumsajili Msuva kwa muda mfupi aweze kuwaongezea nguvu msimu ujao hasa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msukumo mkubwa ukitoka kwa benchi lao la ufundi kwani wamepania kucheza soka la kasi zaidi ya msimu huu na wanaamini Msuva ndiye mtu sahihi kwa Mayele.

Lakini sasa inaelezwa Nabi atalazimika kumtegemea Morrison ambaye wamempa masharti magumu lengo ikiwa ni katika kuboresha kiwango chake na nidhamu ya nje na ndani ya uwanja.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz