Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki amekiri kuwa amepokea ujumbe mwingi mbaya kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya USM Alger.
Mchezo huo Yanga ilipoteza kwa kichapo cha mabao 2-1 na kufanya mashabiki wengi kutoridhishwa na kiwango cha Aziz KI na kumtupia lawama lukuki staa huyo raia wa Burkina Faso aliyenunuliwa kwa pesa ndefu pale mitaa ya Jangwani.
“Ni kweli nimepokea ujumbe mwingi mashabiki wakilalamika juu ya kiwango changu. Ni jambo zuri kwangu kuona mashabiki wanategemea kitu kikubwa kutoka kwangu na siku wasipoona wana haki ya kuongea.
“Nashukuru Mungu tuna mechi nyingine kesho hapa Algeria, hii ni nafasi nyingine kwangu kama mchezaji kuingia uwanjani kwenda kupambana kuhakikisha naisaidia timu kupata ushindi na ninawapa furaha mashabiki wetu,” alisema Aziz Ki.
Kesho Juni 3, 2023, Yanga itaingia uwanjani kutupa karata yake ya mwisho dhidi ya USM Alger kusaka ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika katika Dimba la Julai 5 nchini Algeria.