Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz Ki: Mudathir ana mguu wa dhahabu

Mudathir Yahya Simuu Aziz Ki: Mudathir ana mguu wa dhahabu

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati watu wengi wakimmwagia maua kiungo Mburkina Faso wa Yanga, Stephene Aziz Ki kwa kazi kubwa anayofanya uwanjani, staa huyo amesema mtaalamu zaidi kwenye timu hiyo kwa sasa ni Mudathir Yahya.

Aziz ambaye amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akiongoza kwa kupachika mabao kwenye ligi baada ya kufunga 10, juzi alikimbia na kwenda kumfuta kiatu Mudathir alipofunga bao la kwanza dhidi ya CR Belouizdad na amesema staa huyo wa Zanzibar Heroes ana mguu wa dhahabu.

“Mudathir alipofunga bao la kwanza nilienda kubusu kiatu chake. Yule jamaa ana mguu wa dhahabu kwani tulitumia zaidi ya dakika 40 kutafuta bao bila mafanikio hadi alipofunga yeye kitaalamu. Ni mchezaji hatari zaidi kikosini, anaweza kucheza maeneo tofauti na kufanya vizuri.

“Kuna muda alicheza kama namba sita, wakati mwingine namba na nane na hata namba 10 na huko kote anacheza kwa ubora wa hali ya juu, huo ndio utofauti wake na wengine kwani anafanya vitu vingi ambavyo kila kocha atapenda,” alisema Aziz Ki aliyefunga bao la pili kwenye ushindi mabao 4-0, ilioupata Yanga mbele ya Belouizdad Jumamosi huku mabao mengine mawili yakifugwa na Kennedy Musonda na Joseph Guede.

Staa huyo aliyewika na timu ya taifa ya Burkina Faso kwenye fainali za Afcon 2023 zilizomalizika Februari 13, kwa wenyeji Ivory Coast kutwaa ubingwa alimalizia kwa kusema pamoja na Mudathir kuwa bora lakini pia ubora na maelewano ya kikosi kizima cha Yanga ndio nguzo ya mafanikio kwa timu hiyo.

“Kila mchezaji anacheza kwa kumtegemea mwingine. Yanga ina kikosi bora hivyo hiyo ni faida kwa kila mmoja wetu, hauwezi kuwa bora kama hauchezi na watu bora, hivyo ndivyo soka lilivyo na kinachotubeba zaidi ni muunganiko, umoja na mshikamano tulionao kama timu,” alisema.

Mudathir aliyejiunga na Yanga msimu uliopita katika kipindi cha dirisha dogo kama mchezaji huru baada ya kuachana na Azam, amekuwa na mchango mkubwa kikosini hapo. Staa huyo wa zamani wa KMKM ya Zanzibar amekuwa mhimili wa safu ya kiungo ya Yanga chini ya makocha wote wawili, Nasreddine Nabi aliyeondoka na Miguel Gamondi anayeinoa timu hiyo sasa ambayo imetinga hatua ya robo fainali ya CAF.

Mudathir ambaye pia ni kiungo tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, hadi sasa ameifungia Yanga mabao sita na asisti mbili kwenye ligi na moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mudathir alisema siri ya ubora wake kikosini Yanga ni kufuata maelekezo na kujituma zaidi: “Kiungo Yanga kimesheheni mastaa wenye uwezo hivyo ni chachu kwangu kupambana zaidi na kuonyesha ubora wangu kati yao,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: