Yanga msimu huu imezidi kuwa moto. Inasaka taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara. Ndani ya kikosi chake kuna mastaa wa nguvu na wameifanya kugawa vichapo Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika ambako imefuzu hatua ya robo fainali.
Kazi kubwa ya nyota wa timu hiyo chini ya kocha ni kuhakikisha wanafika mbali zaidi. Mmoja wa mastaa hao ni Stephanie Aziz KI, raia wa Burkina Faso.
Ubinifu wa miguu umemtambulisha kuwa kiungo mshambuliaji fundi nchini. Mikwaju ya friikiki, penalti, matobo na chenga za maudhi ni vyake. Utafurahi kumuona. Utatamani achezee timu unayoishabikia ili umfurahie kwenye kila mechi.
Aziz KI yuko kwenye moto msimu huu pengine tangu atue nchini. Ana mabao 11 kwenye Ligi Kuu Bara moja nyuma ya Feisal Salum ‘Feitoto’ anayeongoza kwa ufungaji akiwa na 12. Kiwango chake kimelilazimisha Mwanaspoti kumsaka na kufanya naye mahojiano mafupi juu ya jinsi alivyojipanga msimu huu na mambo mengine. Twende pamoja.
SIRI YA GAMONDI
Aziz Ki anasema kilichomfanya awe tofauti na msimu uliopita ni kuzoea mazingira na wachezaji wenzake. Lakini kubwa ni kujiamini alikoongezewa na kocha Miguel Gamondi akimwamini na kumpa nafasi nyingi zaidi.
“Gamondi ni kocha mzuri wakati wote anaponipa nafasi najua anaamini nitakwenda kufanya vizuri. Pamoja na kufunga inaniongezea nguvu,” anasema Aziz KI mwenye asili ya Ivory Coast.
“Wakati anafika (Gamondi) tulizungumza kwa kina akanipa mipango yake juu yangu. Kuna mambo ambayo sitaweza kuyaweka wazi, lakini kikubwa kuna nguvu aliihitaji kutoka kwangu. Yapo mambo ambayo alinipangia akitaka aone nayatekeleza, nikaona yapo ndani ya uwezo wangu ndio maana mnaona nilivyo hivi kwa sasa.”
UTATU WAMPA VAIBU
Nyota huyo anasema utatu na wachezaji wenzake kutoka Asec Mimosas kina Pacome Zouzoua na Yao Attohoula umemfanya aongeze uwezo na mara nyingi wamekuwa wakimpa hamasa.
“Yao na Pacome muda mwingi wananiambia kaka unaweza na mimi nikiangalia kile wanachokitoa kwa timu najiona nina deni la kufanya zaidi yao kwa kuwa mimi ni mwenyeji wao hapa. Hivyo wakiwepo uwanjani ni rahisi kupata mafanikio kwani tunajuana na kufahamiana kiuwezo na kimawasiliano,” anasema.
“Kuna nafasi nikipata najua Yao anaiweza, hivyo nampa pasi haraka na kwa Pacome pia, hali inayofanya mechi nyingi tunazokuwepo wote kumalizika vizuri kwani hakuna kinachoharibika.”
HATAKI KIATU
Kiungo huyo ambaye anawania kiatu cha ufungaji bora akiwa na mabao 11 anaeleza kuwa hana mpango na kiatu cha ufungaji bora msimu huu kwani sio mshambuliaji.
Anasema shauku yake ni kuona timu inapata ushindi iwe kwa kufunga au mwingine kwani mafanikio yake yamebewa na kikosi kizima. “Nikianza kuwaza kuhusu kiatu nitakuwa mbinafsi kila mechi nitataka kufunga, hivyo nitakuwa najipambania na sio kuipigania timu tena ili tu niweke rekodi.
“Hivyo sina malengo na kiatu, labda kije chenyewe. Nawaomba watu wasitegemee sana kuhusu hili. Malengo yangu ya msimu huu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kimataifa. Pia kutetea mataji yaliyobaki. Kuhusu kufunga nitafunga kwa kadri Mungu atakavyonijalia huku nikiendelea kupambana kwa ajili ya Yanga.”
YANGA NOMA
Staa huyo anayevaa jezi namba 10 anasema anaiona mbali klabu hiyo kwani malengo ya kila siku yanazidi kuwa makubwa, jambo linalompa furaha kila mchezaji kujiona yupo sehemu salama.
Anaeleza kuwa msimu uliopita walifika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika kama utani kutokana na ubora wa wachezaji na kocha.
“Msimu huu ni balaa, kwani hatukutarajiwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini tumefika na taratibu tutaingia nusu na fainali kwani hilo linawezekana,” anasema
“Usajili mzuri wa msimu huu unatupa uhakika wa kusonga mbele. Msimu uliopita washambuliaji ndio walikuwa wanategemewa sana kufunga, lakini msimu huu viungo wana hatari zaidi, hivyo lolote linaweza kutokea kwani wafungaji ni wengi na timu inazidi kuwa bora.”
SIRI YA MATOBO
Sio rahisi Aziz amalize mechi hajampiga mtu tobo na hilo limempa umaarufumwingine kwa namna anavyowatesa wenzake.
Anaeleza sababu ya kuwa mchezaji ambaye anapiga matobo sana wenzake kuwa: “Hiyo ndiyo aina yangu ya uchezaji wa soka na ninaufurahia na huwa naitumia sana ninapokabwa na wapinzani. kKwa hiyo njia nyepesi ni kuwatoka kwa kuwapiga matobo na kuukimbilia mpira mbele. Napenda sana kupiga matobo kama ambavyo mashabiki wanapenda.”
GUEDE, NYIE SUBIRINI
Aziz anasema mabao ambayo ameanza kufunga mshambuliaji mpya wa Yanga, Joseph Guede ni kama trera tu kwani bado hajaanza kuuwasha moto anaoujua.
Guede aliyetua dirisha dogo msimu huu, alifunga bao katika mechi ya kwanza ya kimataifa dhidi ay CR Belouizdad, huku akiwa nayo mawili katika FA.
Aziz anaeleza kuwa uwezo atakaouonyesha utaendelea kuwashangaza kwani anamjua mshambuliaji huyo vizuri, wakati akiwa FAR Rabat alikuwa akienda Ivory Coast kwa ajili ya mapumziko na walikuwa wakifanya mazoezi na aliwahi pia kumfuatilia kwa ufupi.
“Sina wasiwasi kwani atafunga sana ila alihitaji muda wa kuzoea mazingira na namna ya uchezaji, pia watu wasisahau alikuwa nje kwa muda mrefu,” anasema.
YANGA BINGWA
Aziz anasema licha ya Yanga kuanza msimu kwa kupoteza Ngao ya Jamii kwa watani zao Simba, lakini haoni kama timu yao inaweza kuzuiwa kuchukua ubingwa wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu. “Naheshimu ushindani na timu zingine lakini sioni kama kuna timu inaweza kutuzuia kuchukua tena ubingwa. Tuna kikosi imara na benchi la ufundi imara, lakini zaidi ya yote angalia ambavyo uongozi wa timu yetu na hata mashabiki walivyo pamoja nasi. Hili linatupa nguvu kazi yetu ni moja tu kuipigania timu kushinda,” anasema.
MKATABA MPYA
Mkataba wake unafikia ukingoni mwisho wa msimu na hapa anasema hana tatizo la kubaki Yanga na uongozi wa Yanga uko kwenye mazungumzo mazuri na wanaomsimamia.
“Ni kweli mkataba wangu utafikia mwisho msimu huu, lakini moyo wangu una furaha ya kuwa sehemu ya familia hii ya Yanga. Bado uongozi wangu upo kwenye mazungumzo na uongozi wa Yanga, kila kitu kikimalizika nadhani mambo yatakuwa wazi, “anasema.