Yanga iko kambini na kikosi kizima ambacho kinajiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, staa wa Mabingwa hao wa Tanzania Stephanie Aziz KI ametoa matumaini makubwa.
Katika mahojiano na Mwanaspoti kwenye kambi ya Yanga Jijini Dar es Salaam, Aziz Ki aliuliza hivi; "Nani katoka salama hapa Dar?"
Haishii hapo Aziz KI akaenda mbali akieleza kuwa kwa kikosi chao cha msimu huu kinachomfanya kila staa wa timu hiyo kutolala ili asipoteze nafasi basi ndio mziki itakaokutana nao Belouizdad.
Aziz KI aliyefunga mabao 10 kwenye ligi ameliambia Mwanaspoti kuwa, Belouizdad ilishinda kwao dhidi ya Yanga na sasa inakuja Benjamin Mkapa uwanja ambao timu yao haijapoteza mechi yoyote na wakitaka kuendeleza rekodi yao hiyo katika mchezo huo muhimu wa kufuzu uliobeba matumaini ya klabu na nchi.
Aziz KI aliongeza kuwa maandalizi yao kambini yanatosha kumpa imani kwamba Waarabu hao watakuwa na dakika 90 ngumu mbele yao kwani kitu ambacho wanatamani kukiona kinabaki kwa mashabiki wao ni ushindi.
"Nadhani kilichotokea kwenye mchezo wa kwao kule Algeria kila mmoja kilimuumiza na sasa wanakuja (Belouizdad) wanakuja kwetu nyumbani, nani ametoka na ushindi hapa msimu huu?," alihoji Aziz KI ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Yanga.
"Huu ni mchezo ambao ukiacha kuhitaji ushindi lakini tunataka kuwathibitishia sisi sio wanyonge wao, tutahitaji ushindi ubaki kwa mashabiki wetu wa Yanga, kitu ambacho nataka kuwaambia mashabiki wawahi uwanjani tuanze wote mechi wakiwa wamefurika.
"Imani yangu ya ushindi inatokana na kikosi chetu, nimekuwa hapa kwa miaka miwili sasa lakini hii timu ya msimu huu ni kubwa sana, kila mchezaji hataki kupoteza imani yake kwa makocha ndio maana kila mmoja anapambana ukizubaa mwingine anatumia nafasi yako.
"Tunastahili kucheza hatua ya robo fainali na kwa kuanzia tunatakiwa kuendelea kushinda Jumamosi, tunachohitaji kwanza ni ushindi idadi ya mabao tutajua uwanjani," aliongeza.
Kwenye mchezo wa kwanza Yanga iliondoka kichwa chini baada ya kuchapwa mabao 3-0 lakini baadaye ikashinda nyumbani mechi moja na kutoa sare mbili nyumbani na ugenini.
Yanga iko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi 5, sawa na Belouizdad iliyo katika nafasi ya pili kwa tofauti bora ya mabao ya kufunga na kufungwa huku kileleni wakiwapo mabingwa mara 11 wa michuano hii, Al Ahly ya Misri wakiwa na pointi 6 baada ya zote kucheza mechi nne kila moja.
Timu ya wananchi italazimika kucheza kiwerevu sana ili isiingie kwenye mtego wa kule Algeria ambako ililala 3-0.
Licha ya kutawala mpira kule, Yanga iliingia kwenye mtego mashambulizi ya kushtukiza yaliyoifanya mechi ionekane waliocheza mpira ni wengine na walioshinda ni wengine kwani wanajangwani walitembeza boli ile mbaya, lakini hatari zote zilikuwa langoni mwao kwa makaunta ya kibabe sana ya Belouizdad.
Belouizdad ilipata bao la mapema katika dakika ya 10 kupitia kwa Abdelraouf Benguit na kuitikisha Yanga, kisha katika dakika ya pili ya majeruhi kabla ya mapumziko (45+2) ikaweka la pili kupitia kwa Abderrahmane Meziane na dakika ya nne ya majeruhi kabla ya mechi kumalizika (90+4) wakaweka chuma cha tatu kupitia kwa Lamin Jallow.
Yaani zile dakika za kuzubaa kudhani kwamba mechi imeisha ama mapumziko yamewadia jamaa wanakuweka. Huu mtego uliwadhuru sana Yanga na hawapaswi kujisahau hivyo tena kwa Mkapa Jumamosi.