Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz Ki, Chama wamepata walichostahili

Chama Aziz Aziz Ki, Chama wamepata walichostahili

Fri, 11 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchuma janga hula na wakwao. Itakuwa hivyo kwa mastaa wawili wa Yanga na Simba ambao wamekipata walichokuwa wanakitaka.

Mashabiki watakosa kuona zile burudani zao kwenye mechi tatu kutokana na makosa ambayo waliyafanya jambo ambalo limetibua mipango ya benchi la ufundi kwa timu hizo.

Stephane Aziz Ki na Clatous Chama, watakosekana kwenye dakika 270 ambazo ni mechi tatu, baada ya kufungiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kosa la kukwepa kusalimiana.

Hayo yalifanyika kwenye Kariakoo Dabi iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, Oktoba 23, mwaka huu na ubao ukasoma Yanga 1-1 Simba.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, bao la Yanga alifunga Aziz Ki kwa pigo la faulo, huku kwa upande wa Simba, Chama alimpa pasi Augustine Okrah, akafunga bao.

Mbali na mastaa hao kukosekana kwenye dakika hizo 270, wametozwa faini ya shilingi laki tano kila mmoja kwa kosa hilo.

Hapa Spoti Xtra linakuletea mipango iliyotibuliwa na nyota hao msimu huu.

MAPIGO HURU

Nyota hawa kazi yao kubwa kwenye timu zao ilikuwa ni kwenye upigaji wa mapigo huru, hivyo kukosekana kwao kutalifanya benchi la ufundi kuwatumia nyota wengine.

Aziz Ki na Chama wote wametupia kutokana na mapigo huru. Aziz Ki alifunga kwa faulo dhidi ya Simba, huku Chama akifunga kwa pigo la penalti dhidi ya Geita Gold.

Aziz Ki kwenye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania alipiga jumla ya kona 8, alipiga faulo 4 sawa na zile alizopiga mchezo dhidi ya Coastal Union.

Chama kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold alipiga faulo tatu na penalti moja, mchezo dhidi ya Prisons alipiga faulo tano na kona moja, hivyo kukosekana kwao kumetibua mipango ya benchi la ufundi.

HAPA WALIWATIBULIA WAPINZANI

Wakati Simba ikipambana kutibua rekodi ya Yanga kucheza mechi bila kufungwa na Yanga wakihitaji kuitungua Simba, mpango ulianza kuonekana kujibu kwa Msimbazi dakika ya 13 kupitia kwa Agustine Okrah aliyefunga bao kwa pasi ya Chama.

Kabla hawajaenda mapumziko, Aziz Ki alitibua mipango kwa kufunga bao lililotibua furaha ya Wanasimba, hivyo kwenye mchezo huo wa dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa Oktoba 23 kila mmoja alitibua mipango ya wapinzani wake.

PASI ZA MWISHO

Ile vita yao ya kuwatengenezea washambuliaji wao mabao sasa imetibuliwa kwa dakika 270 ambapo Aziz Ki ana pasi moja ya bao na Chama anazo tatu.

Mipango yao imetibuliwa na itawabidi wasubiri mpaka watakaporejea uwanjani kurejesha makali yao.

DAKIKA ZAO KUGANDA

Hakutakuwa na mwendelezo wa dakika zao za kutumika uwanjani kwa kuwa watakuwa jukwaani mpaka watakaporejea wataendelea kuongeza mwendo kwenye dakika zao.

Aziz Ki ni mechi 7 kacheza akiwa ameyeyusha dakika 468, katupia mabao mawili na pasi moja ya bao.

Chama alikuwa ameyeyusha dakika 712 baada ya kucheza mechi 8 akitupia bao moja na pasi tatu za mabao.

KETE TATU ZA CHAMA

Singida Big Stars (Novemba 9)

Ihefu (Novemba 12)

Namungo (Novemba 16)

KETE TATU ZA AZIZ KI

Kagera Sugar (Novemba 13)

Singida Big Stars (Novemba 17)

Dodoma Jiji (Novemba 22)

Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba, alisema kukosekana kwa Chama kunatibua mipango ya timu hiyo kutokana na umuhimu wa kila mchezaji kwenye kikosi chake.

“Kama una mtoto akaguswa jichoni akaumizwa unadhani utapenda? Haiwezi kuwa hivyo, Chama ni mchezaji wa Simba, anapaswa kutimiza majukumu ya Simba, kukosekana kwake maana yake kuna mipango itavurugika, lakini wapo wachezaji wengine watacheza,” anasema Mgunda.

Kwa upande wa Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga, hivi karibuni alisema kuwa kila mchezaji anapokosekana kwenye kikosi humlazimu kubadili mpango kazi.

“Anapokosekana mchezaji mmoja ambaye huwa anaanza kwenye timu kinachofanyika ni kubadili mpango kazi kwenye mechi husika,” anasema Nabi.

Aziz Ki na Chama kila mmoja amefungiwa mechi tatu za Ligi Kuu Bara na faini ya shilingi laki tano.

Aziz Ki amefunga mabao mawili kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Chama msimu huu kwenye ligi amehusika katika mabao manne, akifunga moja na asisti tatu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live