Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz KI hajazifunga saba tu

Aziz KI Saba Tu Aziz KI hajazifunga saba tu

Mon, 18 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na mechi ya jana usiku wakati kikosi cha Yanga kilipovaana na Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini unaambiwa kiungo Stephane Aziz Ki ni kama anachezea sifa kwa sasa kutokana na rekodi ya mabao kumbeba, akiwa amezinyoosha karibu timu zote isipokuwa saba tu katika ligi hiyo.

Kabla ya mechi za jana hesabu zilikuwa zinaonyesha katika misimu miwili ya kucheza kwake Ligi Kuu Bara, alikuwa ametupia kambani mabao 22, lakini akishindwa kuzitungua timu saba kati ya 15 zinazochuana na Yanga kwa sasa na hata zile zilizoshuka daraja msimu uliopita alipofunga mabao tisa.

Wakati kikosi cha Yanga kilipokuwa kikijiandaa kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuvana na Azam, mwamba alikuwa na mabao 13 akiwa ndiye kinara wa orodha ya wafungaji na ukichanganya na yale ya msimu uliopita yamemfanya awe na mabao 22.

Mabao hayo 13 ya msimu huu amefunga katika mechi 16 kati ya 19 ilizokuwa zimecheza timu hiyo kabla ya mchezo huo wa jana, kwani alikosekana kwenye michezo mitatu dhidi ya Kagera Sugar ulioisha kwa suluhu, Dodoma Jiji ambao Yanga ilishinda bao 1-0 na ule wa 2-1 mbele ya Mashujaa.

Kwa mujibu kwa takwimu hizo, Aziz Ki hajazifunga timu saba pekee katika misimu yote miwili aliyopo katika ligi hiyo, zikiwamo Polisi Tanzania, Mbeya City na Ruvu Shooting zilizoshuka daraja msimu uliopita, huku ikishindwa kuzifunga Coastal Union, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Mashujaa.

Kwa msimu huu, rekodi zinaonyesha Aziz Ki amezifunga Simba, Azam FC, Singida Fountain Gate, Mtibwa Sugar, Namungo, Tabora United, Geita Gold, JKT Tanzania, KMC na Ihefu FC, baadhi akishindwa kuzifunga msimu uliopita kabla ya kujisahihisha msimu huu.

Mwanaspoti linakuletea rekodi za kiungo huyo mshambuliaji ambaye ni msimu wake wa pili ndani ya kikosi cha Yanga akifunga jumla ya mabao 22 huku Azam na Simba zikiwa ni timu alizozifunga misimu yote miwili. Ihefu iliyomgomea msimu uliopita ameitungua safari hii kwenye ushindi wa mabao 5-0.

AZAM NA MTIBWA

Katika misimu miwili mfululizo ya kucheza Ligi Kuu, Aziz KI amezionea zaidi timu za Azam FC na Mtibwa Sugar kwani kila mmoja ameitungua mabao manne.

Aziz KI aliifunga katika mechi zote za Mtibwa msimu uliopita na safari hii ameitungua mara mbili, wakati kwa Azam alianza kuifunga bao moja msimu uliopita na zilipokutana msimu huu ameipiga hat trick wakati Yanga ikishinda 3-2 na jana timu hizo zilikuwa zikirudiana na matokeo bila shaka tayari mnayo.

Timu inayofuata kwa kuifunga mabao mengi ni Kagera Sugar aliyoitungua katika mechi moja tu ya msimu uliopita wakati Yanga ikishinda mabao 5-0 na yeye alipiga hat trick, huku mechi ya duru la kwanza alikwama kama alivyoikosa msimu huu, ingawa wana mechi ya marudiano kufungia msimu.

SIMBA WAMO

Simba imekumbana na dhahma ya Aziz KI akiitungua ndani ya misimu miwili, akifunga bao moja moja, huku nyingine mbili za misimu hiyo akichemsha kukwamisha mpira kambani.

Mnyama ni moja ya timu zilizopigwa mabao mawili na nyota huyo kutoka Burkina Faso, sambamba na Geita Gold aliyoitungua katika mechi zote mbili za msimu huu na Namungo iliyogongwa bao moja kila msimu.

MAAFANDE NAO

Maafande wa JKT Tanzania iliyopanda Ligi Kuu msimu huu imeshakutana na mzimu wa Aziz KI akiitungua bao moja na wana mechi ya marudiano, huku KMC nayo imefungwa moja na tayari imeshamalizana naye.

Tabora United inayocheza ligi kwa msimu wa kwanza imetunguliwa pia bao moja na Aziz KI, kama ilivyo kwa KMC, Singida Fountain Gate na Ihefu.

WAGUMU ASILIA

Tanzania Prisons iliyokutana na Aziz Ki tangu msimu uliopita ni kati ya timu zilizokataa kufungwa na nyota huyo, kwani katika mechi tatu za misimu miwili mfululizo imembania, japo wana mechi ya duru la pili msimu huu na watu wanasikilizia kuona itakuwaje.

Wengine waliokataa kufungwa kabisa na Aziz KI ni Wagosi wa Kaya Coastal Union ambayo tangu msimu uliopita imekuwa wagumu, licha ya kukutana na timu hiyo mara tatu katika ligi na sasa wana mchezo wa marudiano kufunga msimu.

Dodoma Jiji nao wamekuwa wagumu asilia mbele ya Aziz KI kwa kukataa kabisa kuguswa nyavu zao na mchezaji huyo kwani katika mechi nne zote ilizocheza na Yanga wamekutoka salama mbele yake, japo ilipoteza michezo hiyo kwa Vijana wa Jangwani.

Mashujaa inayocheza Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza imeshakutana na Aziz KI lakini ikambania, japo iliruhusu kipigo cha mabao 2-1, kama ilivyokuwa kwa Mbeya City, Polisi Tanzania na Ruvu Shooting hadi zinashuka daraja msimu uliopita na kuipoteza mbele ya Yanga haikuruhusu nyavu zao ziguswe na Aziz KI.

MSIKIE MWENYEWE

Kiungo huyo mshambuliaji ameliambia Mwanaspoti anafurahi kuvunja rekodi aliyokuwa nayo msimu uliopita ya kufunga mabao mengi hadi sasa.

Anasema kiu yake ni kuona anajituma na kuipambania timu ipate matokeo bora na licha ya kufurahia kufunga mabao mengi hadi sasa, kiu yake kuisaidia Yanga kutetea taji la ligi na katika michuano mingine.

“Sijawahi kuzingatia ni timu gani na gani nimezifunga huwa naangalia nimekuwa nikiisaidia timu, kwa namna gani inapata matokeo, nipo tayari kufanya hivyo kwa timu yoyote bila kujali kikubwa ni matokeo mazuri,” anasema Aziz KI na kuongeza;

“Nafurahia kuwa kinara sasa wa upachikaji wa mabao siwezi kuweka wazi ni mabao mangapi nitafunga wala kuzifunga hizo timu ila nikipata nafasi nitafanya hivyo bila kujali,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti