Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz KI anavyojua kuwapa furaha Wananchi

Aziz KI Guard Of Honour.jpeg Stephanie Aziz Ki.

Mon, 27 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bao lililofungwa na mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki katika ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Tabora United liliwanyanyua mashabiki wa timu hiyo na kunogesha sherehe maalumu ya kukabidhiwa kikombe iliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi.

Mashabiki wa Yanga walionekana kupooza kutokana na mshambuliaji wao huyo nyota kupitwa idadi ya magoli na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC, ambao juzi kila mmoja alifikisha magoli 18 na kuifanya vita ya kuwania kiatu cha dhahabu kuendelea kuwa ngumu.

Hata hivyo watani wa Yanga, Simba ambao juzi walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha huenda wakakosa tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kutokana na Azam kujiimarisha katika nafasi ya pili.

Hii ni baada ya ushindi wa mabao 5-1 iliyoupata Azam FC, iliyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, dhidi ya Kagera Sugar.

Wakati hayo yakiendelea, timu ya Mtibwa Sugar imeshuka daraja rasmi baada ya kucheza Ligi Kuu kwa misimu 28, ilipopanda mwaka 1996, ilipokubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Mashujaa FC, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Mabao mengine ya Yanga katika mechi ya juzi yalifungwa na Joseph Guede dakika ya 19 huku Maxi Mzengeli akipachika la pili dakika ya 48 wakati Aziz Ki aliyefunga dakika za majeruhi alimfikia Fei Toto ambaye juzi alipachika mabao mawili.

Magoli mengine ya Azam FC katika mchezo wa juzi yalifungwa na Kipre Junior, Idd Nado na Gibril Sillah, ikifikisha pointi 66 na mabao 61.

Simba, ilipata ushindi wa bao 1-0 ililofungwa na Saido Ntibazonkiza dakika ya pili, lakini uliendelea kuibakisha nafasi ya tatu kwa pointi 66 na bao 57.

Hatima ya timu moja kati ya Simba au Azam kucheza Ligi ya Mabingwa sasa itaamuliwa katika mechi ya mwisho, Mei 28, wakati Wekundu wa Masimbazi watacheza dhidi ya JKT Tanzania na Azam itakuwa Nyankumbu, ikicheza dhidi ya Geita Gold.

Ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, Lake Tanganyika, Mashujaa FC imeichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0, mawili yakiwekwa wavuni na Reliants Lusajo dakika ya tatu na 26, Munhir Viai alitupia la tatu dakika ya 32, bao la kufutia machozi la Wakatamiwa hao yakifungwa na Seif Karihe, ambayo hayakutosha kuwabakisha Ligi Kuu, kwani hata kama ikishinda itafikisha pointi 24, ambazo zimeshapitwa na Geita Gold ambayo ina pointi 25, ikisubiri hatma yake dhidi ya Azam FC.

Coastal Union imeonyesha nia yake ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao ilipolazimisha suluhu dhidi ya JKT Tanzania, na kufikisha pointi 42, ikiwa nafasi ya nne ya msimamo.

Pazia la Ligi Kuu Bara litafungwa rasmi keshokutwa kwa mabingwa kucheza dhidi ya Prisons, Simba yenyewe itawaalika JKT Tanzania, Coastal Union dhidi ya KMC, Dodoma Jiji itawafuata Mashujaa wakati Ihefu itawaalika Mtibwa Sugar na Namungo itawakabili Tabora United.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya Geita Gold FC dhidi ya Azam na Singida Fountain Gate itawakaribisha Kagera Sugar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live