Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz KI amvuruga Fei Toto kabla ya kukutana Jumapili

Fei Toto Amfunika Aziz Ki Ligi Kuu Aziz KI amvuruga Fei Toto kabla ya kukutana Jumapili

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bao la Stephane Aziz KI alilofunga katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, limeifanya Yanga kuendelea kujitengenezea mazingira mazuri ya kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 52 kileleni huku wakiongeza utofauti wa pointi baina yao na Azam (44) pamoja na Simba (42) ambao wapo nafasi ya tatu wakiwa mchezo mmoja nyuma.

Bao hilo lililotokana na asisti ya Augustine Okrah kutokea wingi ya kushoto baada kupiga krosi ya chini, ni la 13 msimu huu kwenye ligi kwa Mburkinabe huyo akiongoza mbio za kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu na kumzidi Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam mwenye mabao 12.

Katika mchezo huo wa 19 kwa Yanga msimu huu kwenye ligi, kocha Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake cha kwanza ikiwemo kumpa nafasi Gift Fred ambaye alicheza sambamba na Bakari Mwamnyeto.

Cha kuvutia zaidi ni namna ambavyo Gamondi aliamua kumtumia Dickson Job katika eneo la kiungo mkabaji ambalo alizoeleka kucheza Khalid Aucho ambaye anauguza majeraha, na beki huyo alicheza vizuri.

Mudathir Yahya, Pacome na Yao walianzia benchi huku nafasi zao wakianza Okrah, Kennedy Musonda na Kibwana Shomary ambaye alipata majeraha na kushindwa kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Yanga ilikuwa bora hasa kipindi cha kwanza ambapo ilitumia maeneo yake ya pembeni kujenga mshambulizi mfululizo lakini nguvu yao ilionekana kupungua kipindi cha pili.

Geita Gold ilionekana kuimarika kipindi cha pili kiasi cha Aziz Ki ambaye alitolewa ilimbidi kusimama akiwa benchi na kuhamasisha wachezaji wenzake.

Kituo kinachofuata kwa Yanga ni dhidi ya Azam FC mchezo ambao utachezwa Jumapili kabla ya ligi kusimama kupisha mapumziko ya kalenda ya FIFA.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live