Wakati Yanga ikirudishwa kwenye uwanja wao wa bahati ulioipa nafasi ya kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, mfungaji wa bao la ushindi Stephen Aziz KI, amesisitiza kuwa wanaenda kusaka rekodi nyingine kwa kupata ushindi utakaowapa mwanga mzuri kwenye kundi lao.
Yanga ambao wapo kundi D, waanatua Tunisia leo kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir ya Tunisia utakaochezwa Februari 12, kisha ikirejea nchini itakuwa na mchezo dhidi ya TP Mazembe na baadaye kuifuata Real Bamako ya Mali.
Aziz KI alisema hatua waliyopo ni ya kusaka matokeo zaidi kwenye uwanja wa nyumbani na ugenini sasa wanaanzia ugenini wanahitaji matokeo ya ushindi au sare ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kujihakikishia kutinga hatua inayofuata.
Alisema kwenye mchezo huo wataingia kwa kuwatazama wapinzani wao kuwa ni bora ili kuwapa heshima ambayo itawafanya waweze kujua ubora au mapungufu ya wapinzani wao baada ya kuanza kucheza hawataingia kwa kujiamini zaidi.
"Tunaingia tikiwaheshimu bila kujali ubora au mapungufu yao lengo letu ni kuhakikisha tunajiandaa vyema muda wa mechi kuanza ndio utakaothibitisha ubora wa timu zote na dakika 90 kuamua nani bora zaidi ya mwingine.
"Hatua tuliyopo inategemea pointi nyingi na mabao ili kuweza kutinga hatua inayofuata hilo tunalitambua hivyo tunahitaji ushindi mzuri nyumbani na hata ugenini ili kujihakikishia pointi ambazo zitatutoa nafasi moja hadi nyingine," alisema KI ambaye ndiye mchezaji staa wa Yanga kwa sasa.
Akizungumzia kucheza uwanja ambao ndio aliipa timu yake matokeo dhidi ya Club Africain, Novemba 9, alisema ni jambo zuri kwa sababu wanaenda kutumia uwanja ambao wanaufahamu baada ya kuutumia dakika 90 bora kwao wanatarajia kucheza kwa kujiamini na kupambana.
"Ni kweli nilipata nafasi ya kufunga kwenye uwanja huo haiwezi kuwa sababu ya kujiamini zaidi tukijua tutashinda tunajiandaa na tunaamini ni mchezo muhimu zaidi kwetu kuhakikisha tunatumia kila nafasi tutakayoipata ili kujiweka salama;
"Kikubwa ninachoweza kusema ni kwamba tunaenda kucheza uwanja ambao tunaufahamu na nchi pia ambayo tumeshafahamu hali ya hewa na mazingira yake hiyo tunaweza kuwa na unafuu kiasi lakini hautufanyi tukashindwa kujiandaa vyema ili kuonyesha ushindani."
Alisema mchezo huo wanauchukulia kwa ukubwa na wanatambua umuhimu wake wao kama wachezaji wamejiandaa kushindana mambo mengine wanaliachia benchi la ufundi kuhakikisha linaboresha na kupanga mbinu bora za kupata ushindi.