Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz KI: Yeyote aje, tumejipanga

Aziz KI 9 Goals Stephen Aziz KI

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Zimebaki saa chache kabla ya miamba ya soka nchini Yanga na Simba kufahamu wapinzani wao kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kiungo fundi wa Yanga, Stephane Aziz Ki amesema wao wala hawana hofu na wanachosubiri kwa hamu ni kusikia watapangwa na nani.

Droo hiyo inatarajiwa kuchezeshwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki, huko Cairo, Misri na itahusisha timu nane zilizotinga hatua hiyo ambazo ni Simba, Yanga, Esperance, TP Mazembe, Al Ahly, Petro Luanda, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas.

Akizungumza na Mwanaspoti, nyota huyo ambaye msimu huu amekuwa moto kwenye Ligi Kuu na hata kimataifa, amesema hawana presha kwani ni lazima wapangwe na yeyote lakini hamu yao ni kujua wanapangwa na nani.

"Kesho 'leo' ni siku ambayo tunaisubiri kwa hamu ili kumtambua mpinzani wetu, sitaki kuzungumzia timu moja moja kwa sababu yeyote tutakayekutana naye lazima tucheze," amesema na kuongeza;

"Yanga ina kikosi kizuri na ipo katika kilele cha kusaka mafanikio, hivyo tunamheshimu kila mpinzani tutakayekutana naye, tukiwa tumejiandaa kushindana," anasema.

Itakavyokuwa. Vyungu viwili katika uchezeshaji wa droo hiyo, cha kwanza kitakuwa na timu nne zilizomaliza nafasi ya pili kwenye makundi yao, huku nyingine nne zitakuwa katika chungu cha pili na ni zile zilizomaliza vinara kwenye makundi yao.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu zilizomaliza nafasi ya pili, haziwezi kukutana katika hatua ya robo fainali kama ilivyo kwa zile zilizomaliza katika nafasi ya kwanza ingawa zinaweza kuumana kwenye nusu fainali au fainali.

Kwenye hatua hiyo ya robo fainali, pia timu zilizomaliza katika nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi zitaanzia nyumbani kwenye hatua hiyo ya robo fainali na zitamalizia ugenini.

Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za Simba, Yanga, Esperance na TP Mazembe wakati chungu cha pili kikiwa na Al Ahly, Petro Luanda, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas.

Kwa kushika nafasi ya pili kwenye kundi B, Simba inaweza kupangwa na mojawapo kati ya Mamelodi Sundowns, Al Ahly au Petro Luanda wakati Yanga iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi D inaweza kukutana na ama Petro Luanda, Mamelodi Sundowns au Asec Mimosas.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: