Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aziz KI, Yao wamtesa kocha Al Merrikh

Aziz Yao Pacome Aziz KI, Yao wamtesa kocha Al Merrikh

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imetinga makundi ikiandika rekodi ya kuing’oa Al Merrikh, kocha wa wapinzani wao amekiri wachezaji waliochangia kuitoa timu yake ni kiungo Stephane Aziz KI, beki Yao Kouassi na Maxi Nzengeli mbali na mabao ya ‘dogo’ Clement Mzize.

Al Merrikh ilifungwa 1-0 kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0, kwani kwenye mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani ilichapwa 2-0.

Akizungumza mara baada ya pambano hilo, Kocha wa Al Merrikh, Osama Nabih alisema hajashangazwa kutupwa nje ya Yanga, kwani wapinzani wao hao wana nyota wasumbufu na wenye uwezo ambao waliwatibulia kila walichokuwa wakikipanga kwenye mechi zote mbili.

Alisema ukimuondoa Maxi Nzengeli, Pacoume Zouzoua na Mzize, lakini watu walioitesa zaidi timu yake ni Aziz KI na Yao kutokana na uwezo walionao wa kuwanyima raha mabeki muda mwingi wa mchezo.

Nabih alisema Yanga ni timu kubwa iliyojengwa vizuri lakini kuna wachezaji wao wawili waliwasumbua kwa uwezo waliokuwa nao akikiri jamaa wanajua sana.

Kocha huyo raia wa Misri alisema walilazimika kutumia nguvu kubwa kumbana Aziz KI baada ya kujua madhara yake tangu mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani hatua ambayo imewasaidia na kukiri Aziz KI ni kiungo aliyekamilika akiwa na ufundi miguuni na mbunifu ambaye atakwenda kuwapa nguvu kubwa Yanga wanapokwenda kucheza makundi.

“Nafikiri tulistahili haya matokeo hatukuwa kwenye ubora kama wenzetu, ukiangalia timu hizi mbili utaona jinsi Yanga walivyo wepesi kushinda sisi wana wachezaji bora sana,” alisema Nabih na kuongeza;

“Unaweza kuona mchezaji kama Aziz KI ni kiungo wa kisasa kabisa, tulipocheza naye mechi ya kwanza tulijua huyu ni mchezaji tunayetakiwa kumchunga sana na hata mikanda ya mechi zao walizocheza nyumbani zilituthibitishia hilo.”

Kocha huyo aliongeza mbali na Aziz KI walijipanga kusaka mabao katika mchezo wa juzi lakini kizuizi kikubwa kwenye ukuta wa wenyeji wao alikuwa Yao.

“Ni beki makini sana ana kasi ya kupandisha mashambulizi lakini pia anakaba kwa umakini sana, huwezi kuamini anachofanya na kimo chake, anacheza kama mwanajeshi muda wote wa mchezo hapungui kasi, Yanga ina wachezaji wengi bora watafanya vizuri wakijipanga vizuri.”

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kuing’oa Al Merrikh kwenye mechi za CAF tangu walipokutana mara ya kwanza mwaka 1973 na kukutana tena 2007 na sasa timu hiyo inasubiri kujua wapinzani watakaovaana nao kwenye makundi baada ra droo itakayofanyika baadaye mwezi huu, huku ikijihakikishia kuvuna kiasi cha Sh 1.8 bilioni

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: