Kiungo wa Yanga, Stephanie Aziz Ki ameibuka kinara wa mabao Ligi Kuu ya NBC akifunga mabao 21 na kumfunika kiungo wa Azam FC, Feisal Salum mwenye mabao 19 wakati ndoto za Simba kushika nafasi ya pili katika ligi hiyo zikiota mbawa.
Kumekuwa na stori kuwa Aziz Ki amegoma kusaini mkataba mpya ndani ya yanga kwa sababu amepata dili kutoka timu kubwa Barani Afrika zikitaka saini yake, lakini mwamba huyo kutoka Burkina Faso amekata mzizi wa fitina akisema kuwa hana mpango wa kuondoka Yanga msimu huu licha ya Eng. Hersi Said (Rais wa Yanga) kumtaka aondoke Yanga baada ya miaka miwili ambayo inatamatika mwisho wa msimu huu.
“Siwezi kumpa zawasi yochote Eng. Hersi kwa sababu amenipa vitu vingi sana tangu alipokuja kunichukua miaka miwili iliyopita. Wakati anakuja alinionesha ‘Aziz nina project hii, ninakuomba uje ufanye jambo kwenye timu yangu”. Niliheshimu project ya Rais na nikaja hapa kwa mkataba wa miaka miwili, ninaweza kuiona project sasa inakoelekea na nina furaha sana.
“Kuna jambo najua yeye amesahau lakini mimi nakumbuka, aliniambia ‘Aziz ninakupa miaka miwili tu, fanya kila kitu kisha baada ya hapo ondoka, baada ya miaka miwili hata mimi nitakutafutia timu uondoke.’ Lakini leo nina furaha kwa sababu project haijakamilika, najua aliniambia baada ya miaka miwili niondoke lakini sitaondoka nitaendelea kubaki kwa ajili ya heshima yake.
“Kwa hiyo ninakuambia boss kwamba asante sana kwa hii nafasi na asante kwa kila kitu kwa sababu umenisaidia sana kuwa bora na hii nizawadi yangu kwako,” amesema Aziz Ki na kumpa Eng. Hersi mpira aliozawadiwa baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Tanzania Prisons ambapo hata hivyo Hersi alimwambia autunze mpira huo kwa ajili yake.