Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam yaizidi akili Simba

Azam Vs Simba 2222 Azam yaizidi akili Simba

Sun, 4 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Azam FC wajanja sana. Ni kama vile ilikuwa inajua kuwa mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba itapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Dar es Salaam na fasta ilianza kujiweka tayari kabla ya juzi kutolewa taarifa rasmi kwamba mechi hiyo itaenda kupigwa huko siku ya Februari 9.

Ipo hivi. Azam karibu wiki nzima sasa imekufa ikipiga tizi kule Azam Complex, kwenye uwanja wa nyasi halisi, zinazofanana na uwanja wa CCM Kirumba utakaotumika kwa mchezo huo maarufu kama Mzizima Derby ambao uliahirishwa mara mbili tofauti kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na Fainali za Afcon 2023.

Hata hivyo, baada ya kupangwa kwenye ratiba ya mechi za viporo, ulikuwa haujaainishwa utapigwa uwanja gani, kwani wenyeji ni Simba ambao uwanja wa nyumbani wa Uhuru na Benjamin Mkapa vyote vimefungiwa na serikali inavyovimiliki na kufanya ianza kusaka viwanja vipya kabla ya juzi jioni kuelezwa utapigwa Mwanza.

Lakini wakati Simba ikikuna kichwa kujua mechi hiyo ikapigwe wapi, Azam ni kama walishituka mapema suala la uwanja kwani katika mazoezi yao walikuwa wakitumia viwanja viwili tofauti, wakwanza ukiwa ule wa nyasi bandia na mwingine ukiwa ni ule wa nyasi za kawaida uliopo viunga vya Azam Complex.

Akizungumzia uwanja, Kocha Mkuu wa Azam, Youssouf Dabo alisema walijiandaa mapema kukabiliana na uwanja wowote ndio maana hata mazoezi wamekuwa wakifanya katika viwanja tofauti.

"Uwanja bora ni hitaji la kila timu, lakini kutokana na mazingira ni ngumu kuwepo na viwanja vizuri kila sehemu. Kwa kutambua hilo tunajiandaa kwaajili ya viwanja vyote na ndio maana huwa tunafanya mazoezi kwaajili ya viwanja tofauti," alisema Dabo anayeendelea kukinoa kikosi cha Azam Jijini Dar es Salaam.

Wakati ikisubiri mechi na Simba, tayari Azam imecheza mechi mbili za kirafiki na timu kutoka Ligi Kuu ya Zanzibar ambapo ilianza kwa kucheza na KVZ Januari 31 mwaka huu katika uwanja wao wa nyasi asilia na kushinda 3-1 kisha juzi kucheza na Mafunzo na kushinda 3-0 na kesho inatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki kabla ya kupaa kwenda Mwanza kuisubiri Simba.

Azam ndio vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa sasa licha ya kulingana pointi 31 na Yanga, inabebwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, japo ina mchezo mmoja zaidi kulinganisha na watetezi waliocheza mechi 12 hadi sasa wakati Wanalambalamba wana 13 na Simba iliyopo ya tatu ikiwa na pointi 26 imecheza 11 tu hadi sasa.

Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa na bahati kwa miaka ya karibuni kila inapoenda kucheza CCM Kirumba, lakini itakuwa na kazi mbele ya wapinzani hao ambao mechi ya mwisho ya Ligi Kuu msimu uliopita zilifungana bao 1-1 baada ya mechi ya duru la kwanza Simba kulala 1-0, pia ikipasuka 2-1 kwenye nusu fainali ya Kombe la ASFC.

Chanzo: Mwanaspoti