TIMU ya Azam FC imepanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuishusha Simba baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma walipokuwa ugen-ini dhidi ya JKT Tanzania.
Azam walipata bao hilo la pekee katika dakika ya 21 lililofungwa na Ayoub Lyanga kwa shuti kali akimalizia vyema pasi ya kichwa ya mshambuliaji Obrey Chirwa.
Kwa matokeo hayo, Azam imefikisha pointi 50 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, pointi moja nyuma ya vinara Yanga, ambao wana pointi 51.
Nayo KMC imesogea nafasi ya sita ikifikisha pointi 36 baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Gwambina mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, KMC ilianza kupata bao lake la kwanza dakika ya 50 kupitia kwa Charles Ilanfya akimalizia pasi ya Emmanuel Mvuyekule.
KMC waliongeza bao la pili dakika ya 61 mfungaji ni Emmanuel Mvuyekule ambaye alimalizia pasi ya Charles Ilanfya, huku wakiongeza la tatu katika dakika ya 71 kupitia kwa Ally Ramadhan kwa shuti la mbali na kuhitimisha dakika 90 wakiwa mbele kwa mabao 3-0.