Timu ya Azam imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya usiku huu kuendeleza wimbi la ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Kagera Sugar 'Wanankurukumbi' katika mchezo mkali na wa kuvutia uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Mabao ya Azam yamefungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya '9, Prince Dube dakika ya 11, Pascal Msindo dakika ya 45 na Alassane Diao dakika ya 84 na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya pointi 31 katika michezo 13 iliyocheza hadi sasa.
Pointi hizo 31 ilizonazo Azam zinaifanya kuendelea kujikita kileleni na kuiacha Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo ikiwa na 27 ingawa imecheza michezo 10 ambayo ni mitatu pungufu ya vinara hao kwa sasa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Bao la leo la kiungo mshambuliaji, Feisal Salum linamfanya nyota huyo kufikisha jumla ya mabao manane ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho msimu huu akipitwa moja tu na kinara wa Yanga, Stephane Aziz KI anayeongoza akiwa amefunga tisa.
Ushindi wa Azam unaifanya timu hiyo kufikisha jumla ya michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 3-1, dhidi ya Namungo Oktoba 27, mwaka huu kwenye uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi.
Kwa upande wa Kagera Sugar inafikisha michezo minne mfululizo bila ya kushinda tangu mara ya mwisho iliposhinda mabao 2-1, dhidi ya Tanzania Prisons Novemba 3, mwaka huu hivyo kuifanya kuchezea kichapo cha sita kati ya michezo yake 13.
Katika michezo 13 iliyocheza Kagera, imeshinda mitatu tu, sare minne na kupoteza sita ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake 13.