Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam yainyoosha Singida, yaipumulia Yanga kileleni

Kipreee.jpeg Azam yainyoosha Singida, yaipumulia Yanga kileleni

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Azam FC imepata ushindi wa kwanza katika mechi tatu ilizocheza ugenini baada ya kuichapa Singida Fountain Gate kwa bao 1-0 kwenye mchezo mgumu uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ukiifanya iipumulie Yanga iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, licha ya kucheza mechi mbili zaidi dhidi ya vinara hao.

Bao la dakika ya 52 la kiungo mshambuliaji Kipre Junior aliyeunasa mpira kutoka kwa beki wa Singida, Yahya Mbegu lilitosha kuwapa ushindi matajiri hao wa Chamazi na kuifanya ifikishe pointi 40, tatu pungufu ya ilizonazo Yanga iliyocheza mechi 16, wakati Azam imecheza mechi 18.

Kabla ya ushindi huo uliopatikana kwa mbinde, Azam ililazimishwa suluhu na Tabora United kabla ya kubanwa tena na Tanzania Prisons na kufunga bao 1-0, matajiri hao wakichomoa bao jioni kwa mkwaju wa penalti iliyowekwa kimiani na Feisal Salum baada ya wenyeji kutangulia mapema kwa bao la Eric Okutu.

Baada ya sare hizo mbili mfululizo ugenini, kwenye mechi ya leo Azam ilipambana kiume na kuvuna pointi hizo tatu na kuifanya ikusanye alama tano kati ya tisa katika mechi tatu ilizocheza na kuibakisha katika nafasi ya pili.

Kipigo hicho kimeishusha Singida kwa nafasi moja hadi nafasi ya saba kutoka ya sita ikibaki na pointi 21, huku Prisons iliyoshinda kwa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Tabora United ikipaa juu.

Licha ya kipigo hicho, Singida ilionekana kubadilika mara baada ya kuruhusu bao hilo na kulishambulia vikali lango la Azam na dakika ya 65 almanusura isawazishe baada ya mshambuliaji Francy Kazadi kupiga kichwa akipokea krosi ya Habib Kyombo, lakini mwamuzi wa pili msaidizi alilikataa bao akidai mfungaji kabla ya kufunga alikuwa ameotea.

Azam inayopambana kusaka taji la Ligi Kuu kwa mara ya pili baada ya awali kutwaa msimu wa 2013-2014 ikiwa ni miaka mitano tangu ilipopanda daraja msimu wa 2008-2009, iliivaa Singida ikiwa na msiba wa aliyekuwa daktari wa timu hiyo, Dk Mwanandi Mwankemwa aliyefariki dunia jana na mwili wake unatarajiwa kuzikwa kesho Alhamisi, jijini Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanaspoti