Uongozi wa Azam FC umeanza mchakato wa kusaka kipa mwingine katika dirisha hili dogo la usajili baada ya makipa wawili tegemeo wa timu hiyo, Ali Ahamada na Abdulai Iddrisu kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.
Ahmada, raia wa Ufaransa mwenye asili ya Comoro alipata majeraha ya goti la mguu wa kushoto wakati Azam iliposhinda kwa mabao 5-0 dhidi ya KMC, lakini alicheza mchezo na JKT Tanzania na ndipo maumivu yalipomzidi na kwenda kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.
Kwa upande wa Iddrisu alikwenda pia nchini humo kwa uchunguzi zaidi wa bega la mkono wa kushoto na ndipo hesabu za kutafuta kipa mwingine zikaanza baada ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Youssouph Dabo kuwataka viongozi kufanikisha hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Dabo alisema katika usajili wa dirisha hili hatangalia majina makubwa isipokuwa ataangalia wachezaji watakaoweza kuendana na falsafa zake za ufundishaji kwa haraka na kuleta tija kikosini.
“Kwangu mchezaji mkubwa ni yule atakayeendana na matakwa ya timu - kwa maana ya kuendana na aina ya soka letu tunalocheza. Hilo ndilo jambo kubwa kwa sababu itatusaidia kwa haraka kutengeneza muunganiko wa kikosi chetu kiuchezaji,” alisema.
Wakati Dabo akizungumza hayo, lakini Mwanaspoti limepenyezewa taarifa za kocha huyo kutaka kipa mwingine kwani hataki kuona kiwango cha timu kikishuka huku ikielezwa bado malengo yake ni kumpata Mnigeria, John Noble anayechezea timu ya Tabora United.
Mbali na makipa hao kuwa majeruhi, lakini beki Abdallah Kheri ‘Sebo’ na kiungo Sospeter Bajana ni majeruhi, huku Djibril Sillah akianza mazoezi mepesi baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania.