Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam yaifuata Simba

60966 Azam+pic

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lindi. Baada ya kusubiri kwa misimu mitatu, Azam FC wamehitimisha nuksi waliyokuwa nayo kwenye mashindano ya FA jana, kwa kutwaa ubingwa kufuatia ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Ilulu mjini hapa.

Bao la dakika ya 64 la mshambuliaji raia wa Zambia, Obrey Chirwa akiunganisha mpira uliopigwa na kipa wao, Razack Abalora lilitosha kuipa Azam taji hilo ambalo mshindi wake anapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Wakati Azam wakicheza michuano hiyo mwakani, Simba waliotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara wiki iliyopita watakuwa wakikipiga katika Ligi ya Klabu barani humo.

Katika mchezo wa jana ilionekana mapema tangu kuanza kwa kipindi cha pili kuwa mbinu ya kutumia mipira mirefu ingewanufaisha Azam kutokana na jinsi ilivyokuwa inawapa tabu walinzi wa Lipuli katika uokoaji.

Baada ya kupata wakati mgumu kufumania nyavu katika kipindi cha kwanza wakitumia pasi za chinichini, Azam walibadilika dakika 45 za kipindi cha pili kwa kupiga mipira mirefu kuelekea langoni mwa Lipuli, wakitumia udhaifu wa wapinzani wao hasa mabeki ambao walionekana kuchoka.

Hilo lilijidhihirisha kutokana na bao la Chirwa ambaye mara baada ya kupokea mpira mrefu kutoka kwa Abalora alimzidi nguvu beki Haruna Shamte aliyeanguka na kupiga shuti la chinichini lililomshinda kipa wa Lipuli, Mohammed Yusuph na kujaa wavuni. Hata hivyo, kama Lipuli wasingechoka katika kipindi cha pili pengine mechi hiyo ingelazimika kuamriwa kwa mikwaju ya penati, kwani katika kipindi cha kwanza walionekana kuwabana Azam na kupishana nao mara kwa mara, lakini bahati mbaya kwao walishindwa kutumia nafasi kadhaa ambazo walitengeneza.

Pia Soma

Washambuliaji wa Lipuli kama ilivyo kwa wale wa Azam, kipindi cha kwanza walipata nafasi ambazo kama wangekuwa makini wangeweza ‘kumaliza mechi mapema’ lakini walizipoteza na kushindwa kuzibeba timu zao.

Mfano wa nafasi ambazo zilipotezwa ni ile ya dakika ya 13 ambayo Ngoma akiwa kwenye nafasi nzuri baada ya kupokea pasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alipiga shuti lililotoka nje pamoja na krosi iliyopaa sentimita chache juu ya lango ambayo ilipigwa na Nico Wadada kutoka kulia dakika ya 23.

Shambulizi hilo lilikuja kujibiwa dakika ya 34 ambapo Miraji Athuman wa Lipuli akiwa analitazama lango alipiga kichwa hafifu kuunganisha krosi ya William Lucian ambacho kiliokolewa na Mudathir Yahya na kisha mpira huo kumkuta Paul Nonga ambaye alipiga shuti lililombabatiza mchezaji wa Azam na kuokolewa.

Mchezo huo ulichezeshwa na marefa sita, tofauti na utamaduni uliozoeleka.

Refa wa kati alikuwa ni Hans Mabena aliyesaidiwa na washika vibendera Mohammed Mkono na Ferdinand Chacha, huku kukiwa na waamuzi wa ziada waliokaa nyuma ya kila goli ambao ni Florentina Zabron na Martin Saanya, ilhali Abubakar Mturo alikuwa mezani.

Mara baada ya mchezo beki Aggrey Morris wa Azam alitangazwa mchezaji bora wa mashindano wakati tuzo ya mchezaji bora wa mechi ikienda kwa Paul Ngalema wa Lipuli, ambapo mwenzake Seif Karihe alitwaa tuzo ya mfungaji bora kutokana na mabao manne aliyofunga kwenye mashindano hayo. Mbali na ubingwa na kombe ambalo walikabidhiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Azam pia watapata zawadi ya Sh50 milioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz