Uongozi wa Klabu ya Azam Fc umekiri kuwa wamefanya tathmini na kubaini kuwa wanayo matatizo yao binafsi ambayo yanachangia wao kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Akizungumza na Kipenga ya East Africa Radio kinachosikika kila siku kuanzia saa mbili usiku,Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo Abdulkarim Amin ''Popat'' amesema licha ya kukumbana na kikwazo cha ubora wa vilabu vya Yanga na Simba, lakini zipo sababu zao binafsi ambazo wanashughulika nazo kila siku ili kuzitatua.
''Kila Taasisi ina changamoto zake, sisi tunazo zetu binafsi mfano tumekuwa tukiajili makocha ,tunasajili wachezaji na wasipofanya vizuri ndani ya muda mfupi tunawaondoa, hivyo tunashughulika nazo na tunaamini itafika siku tutakuwa sawa'' Popat amesema.
Katika hatua nyingine, Popat amesema licha ya kusuwaswa katika mechi mbili zilizopita lakini malengo yao yapo palepale na wanaimani na Kocha wao Abdihamid Moallin ambaye tangu achukue mikoba ya kikinoa Azam Fc kimepoteza mechi moja pekee dhidi ya Biashara Mara United.