Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam yaanza kuuza vijana ughaibuni

Azam Ughaibuni Azam yaanza kuuza vijana ughaibuni

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni miaka miwili sasa tangu Kocha Mohammed Badru aamue kujikita kwenye soka la vijana huku matajiri wa Chamazi, Azam FC wakimwamini na kumpa majukumu ya kulea na kuendelea vipaji huku kukiwa na mpango kabambe ambao utaifanya klabu hiyo kujiingia pesa kutokana na biashara ya kuuza wachezaji Ulaya.

Kama ulikuwa na mawazo kuwa malengo ya akademi ya Azam FC ni kwa ajili ya kukilisha kikosi chake cha kwanza, hapana ulikuwa ukijidanganya mpango wa kwanza ni kufanya biashara huko Ulaya, Amerika na kwingineko.

Hilo limefichuliwa na Badru ambaye wakati akikabidhiwa kibarua hicho alielezwa wazi mradi huo ni hadi mwaka 2025 lakini matunda yake tayari yameanza kuonekana ndani ya kipindi kifupi huku akikiri bado anakazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha klabu mbalimbali kwenye mataifa makubwa Ulaya zinavutiwa na wachezaji wao.

Kocha huyo ambaye hilo ni eneo lake na alikuwa akilifanyia kazi kwa miaka mingi tangu akiwa England ambako alihudumu kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya kurejea nchini na kufanya kazi na klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara na Zanzibar.

Kwanini Badru ameamua kurejea kwenye soka la vijana? Kocha huyo anafunguka huku akieleza zaidi majukumu aliyotwishwa na Azam pamoja na mwelekeo wake huku akieleza pia kwa mara ya kwanza sakata lake la vyeti ambalo lilimfanya kuitwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF).

SAKATA LA VYETI

Mwaka mmoja uliopita, sekretarieti ya TFF ilimfungulia mashitaka Kocha Badru mbele ya kamati ya maadili.

TFF ilithibitisha kufungua mashataka hayo kupitia taarifa maalumu iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, ikieleza dhamira ya kufanya hivyo dhidi kocha huyo ambaye aliwahi kuzifundisha Gwambaina na Mtibwa Sugar.

Badru alidaiwa kuwasilisha vyeti visivyo sahihi, hivyo hakuwa na sifa ya kufundisha timu za vijana kwenye klabu za Azam FC hapa kocha huyo anaeleza nini ambacho kilitokea hadi mambo yakawa shwari.

“Niliitikia wito na kwakuwa TFF ndio wazazi wetu kwenye soka la Tanzania mambo yaliisha, niliwaonyesha cheti changu ambacho ilibidi kibadilishwe maana ni UEFA C na huo ukawa mwanzo mpya kwetu na tangu hapo hakuna shida yoyote ambayo ilitokea, zaidi kuna fursa ya kusoma niliipata na nilijiendeleza,” anasema kocha huyo.

ALIVYOINGIA AZAM

Badru anaamini kuna makocha wengi nchini na wenye sifa kubwa pengine kuliko yeye lakini uwezo na uzoefu wake kwenye soka la vijana vilimbeba.

“Nimefanya kazi ya kufundisha vijana kwa miaka mingi sana huku ndipo ambapo nimekuwa nikifurahia, napenda kumtoa mchezaji kutoka sifuri hadi mia, hakuna mtu mwepesi kwenye kujifunza kama mtoto ndio maana nimekuwa nikifurahia kuwalea na kuendeleza vipaji vya vijana wadogo,” anasema.

Wakati akiwa Zanzibar kwa mapumziko baada ya kuinusuru Mtibwa Sugar kushuka daraja mwaka 2021, Badru anasema kuna siku alipokea simu kutoka Azam na kuelezwa mpango walionao kwenye soka la vijana kisha kumtaka kuwa sehemu ya kufanikisha hilo.

“Tulikaa mezani na kufanya makubaliano na mara moja nikaanza kazi,” anasema.

MWANZO NA MAFANIKIO

Ndani ya mwaka wa kwanza, Badru anasema, “Nakumbuka nilikuta vijana 25, nilipewa uhuru wa kufanya ninachotaka, sikutaka kumuondoa kijana yeyote japo wapo ambao niliona uwezo wao uko chini nilijisemea nataka kufanya mapinduzikuinua uwezo wa kila mchezaji ndani ya kipindi kifupi nilifanikiwa kwenye hilo japo wachezaji wawili waliondoka, walishindwa kuendana na kasi yangu.

“Ndani ya mwaka mmoja tulikuwa mabingwa wa Ligi ya Vijana chini ya Miaka 17 bila ya kufungwa mchezo hata mmoja na tuliruhusu bao moja tu, hatukuishia hapo tulishiriki pia kwenye mashindano ya Cambiasso ambayo yalihusisha timu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ufaransa, vijana wangu chini ya miaka 17 ndio walioshiriki katika mashindano hayo ya chini ya miaka 20.

“Tulishahili kuwa mabingwa lakini kwa bahati mbaya tulipoteza kwenye fainali, tulikuwa na wakati mzuri kwenye mashindano hayo na tulionyesha utofauti mkubwa na mwaka uliofuata niliwapandisha na kuwa U20 ambapo tulishika nafasi ya tatu kwenye ligi ya vijana ambao Mtibwa walichukua ubingwa,” anasema.

MPANGO WA AZAM

Badru anasema mpango wa Azam ni kuuza vijana wake Ulaya lakini kwa wale ambao watakwama ndio wataangalia fursa zilizopo nchini wataanza kwa kutolewa kwa mkopo na wale ambao watakuwa na ubora mkubwa, basi watapata nafasi ya kuonyesha makali kwenye kikosi cha kwanza.

“Azam huko nyuma haijawahi kutoa mchezaji kijana kwenda Ulaya au Amerika sio kwa kufanya majaribio namaanisha kusajiliwa moja kwa moja, sasa nguvu iliyopo ni kubwa na bila shaka hilo litaanza kuonekana kwa ukubwa wake japokuwa kwa sasa mambo yameanza kujipa taratibu.

“Yupo mchezaji ambaye tumemuuza, Cyprian Kachwele kwenda Vancouver Whitecaps FC,” anasema kocha huyo.

VIJANA NI BIDHAA

Badru anasema hiki ambacho kinafanywa na Azam kilipaswa kufanywa na klabu nyingine zenye uwezo maana biashara ya vijana imekuwa na faida kubwa sana.

“Vipo vituo na hata klabu nyingi England ambazo nilikuwa nikifanya kazi zimekuwa zikipata pesa nyingi sana kwenye biashara ya soka la vijana.

“Thamani ya vijana wenye vipaji vikubwa ipo juu nadhani kuna haja ya kutazamwa fursa hii, kwani tukizalisha vijana wa kutosha na wenye uwezo mkubwa kesho watakuwa msaada kwa Timu ya Taifa ya Tanzania,” anasema kocha huyo.

KACHWELE AFUNGUKA

Kachwele ambaye anatarajia kwenda Canada kwa ajili ya kuanza maisha yake mapya ya soka alizungumza na Mwanaspoti.

“Kocha Badru ni mwalimu mzuri ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwenye soka langu. Tulianza kwa kufanyia kazi upungufu ambao nilikuwa nayo kiuchezaji, aliniaminisha kuwa naweza kupiga hatua, kwa kweli nashindwa kuamini kilichotokea.

“Nawashukuru sana viongopzi wa Azam FC kwa fursa waliyonipa ya kulea kipaji changu na kuwa sehemu ya kufanikisha ndoto ya kucheza mpira Ulaya.”

Chanzo: Mwanaspoti