Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam wasirudie tena kutoa timu uwanjani

Azam Squad Kikosi cha Azam FC

Sat, 5 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nilipoanza kusikia watu wanajadili kuwa Azam FC wamesusia mechi ya kirafiki huko Tunisia mwanzoni sikuamini sana nikahisi kama stori tu.

Maana mimi naifahamu Azam FC kama miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zikizingatia sana ile dhana kuwa soka ni mchezo wa kiungwana na ndio maana kuna nyakati imekuwa inaonewa lakini haikuwa inaanzisha vurugu au kugomea mchezo.

Baadaye nikajiridhisha kuwa kweli waliamua kutoa timu uwanjani kwa kile walichodai kuwa wapinzani wao walikuwa wanapendelewa na mwamuzi lakini pia wao hawakuwa wakitendewa haki na refa huyo wa mechi hiyo.

Hili jambo binafsi likanisikitisha sana kwa vile sikuona sababu ya kugomea mechi kwani katika soka nyakati kama hizo za timu pinzani kupendelewa huwa zinatokea lakini kwa kuwa mchezo wa soka ni wa kiungwana huwa haishauriwi kufanya uamuzi wa kusitisha kucheza.

Lakini nilitegemea pia Azam FC wangeendelea kukomaa na kucheza mechi hiyo kwa vile ingewapa picha halisi ya namna ya kukabiliana na mazingira kama hayo pindi yanapotokea kwenye mashindano kwa vile huko kuna sheria kali kidogo.

Ukifanya kosa kama hilo kwenye mashindano ni unaweza kushushwa daraja na faini kali ya fedha au kupokonywa pointi na hata kuondolewa mashindanoni, ambazo zote hazipendezi kwa timu yoyote ile ya soka.

Ukiondoa hilo, pia mechi kama hizo za kirafiki zinasaidia kujenga uhusiano baina ya timu na timu au timu na nchi husika sasa unaposusa maana yake hutengenezi mazingira mazuri ya uhusiano bora bali unayumbisha.

Kuna leo na kesho, ambapo Azam wanaweza kurudi Tunisia ambako wanaweza wasitazamwe kwa jicho zuri kutokana na hicho walichokifanya ambacho kilikuwa na uwezekano wa kuepukika.

Tunawapa pole kwa uonevu waliofanyiwa ikiwemo kwa beki wao Charles Edward Manyama kuchezewa rafu mbaya iliyopelekea avunjwe mkono lakini tunaamini haikupaswa kuwa chanzo cha wao kutoendelea na mechi.

Uzuri wa Azam FC ni timu inayoundwa na watu wenye weledi na waelewa hivyo naamini kilichotokea Tunisia hakiwezi kujirudia tena.

Chanzo: Mwanaspoti