Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam wanakosa kitu kisichoonekana kwa macho

Azam Onekanaaaa Azam wanakosa kitu kisichoonekana kwa macho

Tue, 27 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa sasa John Bocco anafahamu. Sure Boy anafahamu. Shomari Kapombe anafahamu. Erasto Nyoni anafahamu. Gadiel Michael anafahamu. Aishi Manula anafahamu. Hata Prince Dube ameanza kufahamu.

Tatizo la Azam ni nini? Watu wamekuwa wakiulizana. Sina jibu lakini naweza kukisia kwamba kuna kitu kisichoelezeka sawa sawa kinakosekana Azam. Labda zinakosekana hisia kali fulani kwa kila anayehusika pale Azam.

Azam hawatembei na madeni ya hisia za watu? Labda. Ndiyo, labda. Wana kila kitu. Uwanja wa kisasa, kambi za kisasa, usafiri wa kisasa, pesa na kila kitu. kwanini watolewe na APR kirahisi namna hii? Wamewekeza pesa nyingi kuliko APR, kwanini watolewe na APR kirahisi namna hii?

Sio kwamba Simba na Yanga hazijawahi kufanya uzembe huu. Hapana, zimefanya. Lakini huwa zinajibu mapigo kwa sababu zinahisi zina madeni makubwa kwa watu. Yanga walitolewa na Rivers United, waliporudi tena kucheza na Rivers wale Wanijeria walikiona chamoto.

Hata Simba waliwahi kutolewa na Jwaneng Galaxy, lakini waliporudi tena katika michuano iliyofuata ya CAF Simba wakaishia robo fainali. Simba na Yanga zinapofanya vibaya nchi inatikisika. Hisia zinakuwa kali. Hata hivyo, Azam wanashindwa kujibu mapigo.

Mara ya mwisho katika michuano ya CAF mwaka juzi tu walitolewa na timu dhaifu kutoka Ethiopia. Tulidhani wamehifadhi hasira kama Simba na Yanga zinavyofanya lakini ndio kwanza wametolewa katika staili ile ile na APR.

Hata hivyo, umeona Azam wanadhihakiwa sana mitandaoni baada ya kutolewa? Umeona kuna vikaragosi vimechorwa mitandaoni kwa sababu ya Azam? Mitandao imekaa kimya na yametokea maneno machache tu ya kuwadhihaki. Hakuna hata presha yoyote ya kumfukuza kocha. Ingekuwa kwa wakubwa hali ingekuwa tofauti.

Ingekuwa Simba au Yanga ametolewa na APR nchi isingekalika. Ni hapa ndipo ambapo wanapata msukumo mkubwa ambao Azam hawana. Ukiwauliza hao wachezaji ambao waliwahi kucheza Azam halafu wakaenda timu za mjini watakwambia.

Presha ni kubwa. Aishi anaishi kwa uchungu sasa hivi. Baada ya kufungwa mabao matano na Yanga anaandamwa. Angekuwa amefungwa mabao yale akiwa katika lango la Azam sidhani kama haya matatizo yangemkumba.

Lakini pia kuna upande wa kusifiwa. Ukicheza hizi timu unasifiwa. Unatukuzwa. Unajikuta unawajibika mara mbili zaidi uwanjani tofauti na ulivyokuwa Azam. Leo Dube akitembea mtaani atasalimiwa na watu ishirini tofauti. Wakati anacheza Azam angeweza kusalimiwa na watu wawili tu.

Msukumo unakwenda kwa kila mtu ambaye anazizunguka Simba na Yanga. Wachezaji wa timu pinzani wanazihofia. APR wangeweza kuhofia zaidi kucheza na Simba au Yanga. Waamuzi pia wanazihofia. Mara ngapi Azam inafanyiwa dhuluma lakini tunaona kitu cha kawaida?

Hata mabosi wanaoendesha mpira huwa wanazihofia Simba na Yanga. Kuna wakati unaona wazi kwamba ratiba inawapendelea. Ndiyo, hisia hizi hazipo kwa Azam. Wana kila kitu lakini wanakosa kitu hiki. Nadhani wanahitajika kuweka pesa nyingi zaidi kuzidi hisia hizi.

Hatujui ni kitu gani Patrice Motsepe na Mamelodi Sundowns yake walifanikiwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa na kusambaratisha kabisa utawala wa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Kwa muda mrefu sasa Ligi imekuwa yao peke yao. Wameweka pesa nyingi katika timu yao lakini sidhani kama wamefanikiwa kubomoea ngome za mashabiki wa klabu hizi.

Labda Azam wawezeke zaidi kiasi kwamba wafanikiwe kabisa kusambaratisha hisia za mashabiki wa Simba na Yanga. Kwamba wawekeze kiasi kikubwa cha pesa kama kile ambacho Mamelodi wameweka katika mpira wao. Labda wawe na wachezaji wa kuanzia dola 500,000 na kuendelea.

Lakini mbona mpaka sasa wana kikosi kikali. Wachezaji hawa hawa waliopo katika kikosi cha Azam leo kama wangekuwa ndio wachezaji wa Simba na Yanga pale Kigali bado wasingeshindwa mechi. Mabasi mengi yangesafiri kutoka mikoa ya Tanzania kusapoti timu yao na wachezaji na viongozi wangejua umuhimu wa mechi iliyopo mbele yao.

Kinachonitatiza zaidi ni kwamba kwa sasa walau Azam imeanza kuambulia chuki kutoka kwa mashabiki wa Simba na Yanga. Nadhani inahusu zaidi kuhusu kuanza kuchukuliana wachezaji kama ilivyokuwa katika sakata la Fei na Yanga. Lakini hapo awali watu wa Simba na Yanga wote walikuwa wanataka Azam ifanikiwe. Bado haikufanikiwa.

Katika Ligi ndipo Simba na Yanga wameweka ubinafsi mkubwa lakini katika mechi za kimataifa wote walikuwa wanataka Azam ifanikiwe. Tatizo ni nini? Labda wenyewe wana majibu zaidi lakini ukweli ni kwamba jambo lenyewe linakatisha tamaa.

Yanga na Simba zimesogea mahali katika michuano hii lakini Azam haionekani kusogea. Wakati huu tukiamini kwamba timu za ukanda huu tumeziweka nyuma, Azam wanatuangusha kwa kutolewa na APR. binafsi nilikuwa nawafikiria zaidi katika pambano lijalo dhidi ya Pyramids lakini wao ndio kwanza wametolewa na timu kutoka Rwanda.

Simba ya msimu uliopita ambayo tuliamini ilikuwa mbovu iliishia robo fainali ya michuano ya CAF. Katika ligi walifanikiwa kuipisha Azam kushika nafasi ya pili lakini katika michuano ya CAF wakawa na mwendelezo ule ule.

Wote tunaamini kwamba Azam ya msimu uliopita ilikuwa kali kuliko Simba. Lakini nani aliishia wapi katika michuano ya CAF? Azam ya msimu huu inatarajiwa kuwa imeimarika kuliko Azam ya msimu uliopita lakini ndani ya raundi ya kwanza tu imetolewa.

Wanaweza kuendelea kutafuta suluhisho lakini kitu kinachochekesha zaidi ni kwamba familia ya Mzee Bakhresa wala haitapokea matusi ya nguoni kutoka kwa mashabiki. Wanaweza kutulia na kunywa kahawa. Lakini kama ndio wangekuwa wanaimiliki Simba au Yanga halafu jambo hili limetokea wangeweza kupata joto kali. Labda shida inaanzia hapa.

Chanzo: Mwanaspoti