Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam wanaitaka kweli nafasi ya pili

Kipre Azam Fc Azam wanaitaka kweli nafasi ya pili

Sun, 19 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amewapongeza wachezaji wa timu hiyo baada ya kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa ushindi wa mabao 3-0, ilioupata juzi Jumamosi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza lakini amebainisha wataanza kuifikiria mechi ya fainali baada ya kumaliza kazi ya kuisaka nafasi ya pili kwenye ligi.

Katika mchezo huo, mabao ya Azam yalifungwa na nyota wa zamani wa Coastal Union, Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyefunga mawili na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Dabo alisema siri kubwa ya ushindi huo ni kutokana na wachezaji kufuata maelekezo yake vizuri na kutumia nafasi vyema kutokana na makosa ya wapinzani wao.

“Tulicheza vizuri na tulistahili kushinda, lakini mchezo huo umekwisha na sasa tunarudi kujipanga kumalizia michezo ya Ligi Kuu Bara iliyobakia kwa sababu pia tuna kazi ya kufanya kisha baada ya hapo ndipo tutageukia fainali,” alisema.

Kwa upande wa Sopu aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo akifunga mabao mawili moja la penalti na lingine akiunganisha kwa kichwa krosi ya Lusajo Mwaikenda, alisema amefurahishwa na jinsi walivyopambana na kufuzu fainali huku akiweka wazi wako tayari kukutana na yeyote.

Ushindi huo umeifanya Azam kulipa kisasi mbele ya Coastal Union kwani msimu wa 2021-2022 zilipokutana nusu fainali Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ilitolewa kwa penalti 6-5, baada ya timu hizo kutoka suluhu dakika zote 120.

Hii ni fainali ya nne kwa Azam FC katika Kombe la FA na mara tatu ilizotinga imechukua mara moja tu, msimu wa 2018-2019, ilipoifunga Lipuli ya Iringa bao 1-0, Uwanja wa Ilulu, mkoani Lindi. Fainali mbili dhidi ya Yanga (2014-2015) na 2022-2023 zote imepoteza.

Tangu kuanza kwa michuano hiyo mwaka 1967 ikifahamika kwa jina la FAT kabla ya 2015 kubadilishwa na kuitwa ASFC, Yanga ndio timu iliyotwaa mara nyingi ubingwa huo ikifanya hivyo mara saba kuanzia 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023.

Azam FC inasubiri mshindi kati ya Yanga na Ihefu zilizokuwa zinacheza jana Alasiri ili kujua itacheza na nani hatua ya fainali itakayopigwa Juni 2, mwaka huu.

Chanzo: Mwanaspoti