Wakiwa ugenini jijini Benghazi huko Libya, Azam FC walifungwa 3-0 na Al Akhdar SC ya huko, na kujiweka kwenye hatihati ya kufuzu raundi inayofuata ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mashabiki wa timu hiyo na Watanzania kwa ujumla wameingia hofu kama kweli timu hii inaweza kubadilisha matokeo katika mchezo wao ya mkondo wa pili.
Wenyewe wameshatangaza kufanya Remontanda, neno lenye asili ya Hispania lenye maana ya kupindua meza au kupindua matokeo.
Wakiwa Chamazi, Azam FC, wanao uwezo wa kupindua matokeo na kusonga mbele wakijituma na kuwa makini. Remontanda inawezekana kweli.
Lakini ni lazima kwanza warekebishe makosa rahisi ya kiufundi yaliyofanywa na benchi la ufundi kule Benghazi.
Katika mchezo wa kwanza, kocha wao, Denis Lavagne, licha ya uzoefu alionao kwenye mashidano ya Afrika, hakuwa na heshima kwa wenyeji wake.
Akijua fika kwamba anawakosa wachezaji wake muhimu kama Malickou Ndoye na Daniel Amoah kwenye safi ya ulinzi, akaingia na viungo wawili tu huku akitumia washambuliaji wawili.
Lavagne alipaswa kujihami zaidi kwa kuweka viungo watatu katikati ili kudhibiti eneo la Kati la uwanja ambalo ndipo mipango ya ushindi hufanyika. Kuanza na washambuliaji wawili hupunguza mizania kwenye timu na kuonekana kupwaya, matokeo yake wapinzani wakawa wanafika kirahisi sana langoni kwao.
Halafu kumuacha Kipre Junior nje na kuanza na Pascal Msindo kwenye wingi ya kushoto, ni dharau nyingine.
Mechi kama ile siyo ya kujaribisha wachezaji, ni ya kutumia wachezaji bora ulionao. Makosa kama haya aliyofanya kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Alimtumia Tepsie Evance kama namba 10 na kumuacha Abdul Sopu ambaye ni bora sana katika eneo hilo. Makosa kama haya yanaweza kukufanya mtu umkosee adabu kocha huyu mwenye mafanikio makubwa Afrika.
Tangu aje Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 2007, Denis Lavagne amecheza mechi 88 za mashindano ya CAF kwa klabu, akifanikiwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2008 na Kombe la Shirikisho 2020.
Huo ni uzoefu mkubwa sana ambao ungeweza kutosha kumfanya awaheshimu Al Akhdar, lakini hakufanya hivyo.
Sasa ili Remontanda iwezekane, ni lazima kuepuka makosa rahisi kama haya.
Ampange Abdul Sopu kama namba 10, nyuma ya Prince Dube.
Ampange Kipre Junior kama winga, na aidha Ayoub Lyanga au Tepsie Evance. Ampange Lusajo Mwaikenda kama namba mbili, na Bruce Kangwa. Lakini kwa Mwaikenda, itategemea na kupona kwa Daniel Amoah au Malickou Ndoye. Remontanda inawezekana, lakini Lavagne awe na heshima kwa wapinzani.