Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam kushusha mashine mpya

Azam FC New Azam kushusha mashine mpya

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya kufunga mwaka kwa ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Mbeya City, Kocha Msaidizi wa Azam, Agrey Morris alisema kama benchi la ufundi watakaa na viongozi kuona wanafanya usajili kwenye eneo linalohitajika.

Azam ilipata ushindi huo ulioifanya ifikishe pointi 40 baada ya mechi 19 kwenye pambano lililopigwa juzi usiku Azam Complex, jijini Dar es salaam kwa mabao mawili ya Abdul Suleiman ‘Sopu’, Prince Dube, Idd Seleman ‘Nado’, Mkenya Kenneth Muguna na Cleophas Mkandala.

Kauli ya Morris inakoleza uvumi wa kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kujiunga na timu hiyo kwani anatajwa kumalizana na mabosi wa Azam na sasa yupo zake nje anakula bata.

Baada ya mchezo kumalizika, Morris alisema kikosi chao ni kipana na kinajitosheleza, lakini benchi la ufundi litakaa na uongozi wa juu kuona wanafanya usajili kwenye eneo lipi, kwani wanataka kuleta mashine katika dirisha hili.

“Tutakaa na viongozi wa juu ili kwenye sehemu ambayo inaonekana kuna tatizo tuongeze mtu, ila kwa sasa kikosi changu kinajitosheleza,” alisema Morris.

Akizungumzia ushindi wao wa kwanza mkubwa kwenye ligi msimu huu, Morris alisema ni walizungumza na wachezaji wao kipindi cha pili wakiwataka kutumia kila nafasi.

“Tulitengeneza nafasi nyingi na kuzitumia ndio maana tumepata ushindi huu, nawapongeza vijana wangu na tunajiandaa kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi,” alisema Morris.

Upande wa Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima alisema matokeo hayo yamewasikitisha kwa sababu ni kipigo cha kwanza kukipata kwenye ligi msimu huu.

“Matokeo haya yametusikitisha na kupoteza kwa kiwango cha mabao haya ni mara yetu ya kwanza lakini tutaenda kujipanga na kuja kivingine,”alisema Mwamlima. Ushindi huo unaifanya Azam iendelee kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 40 katika mechi 19 ilizocheza. Mchezo huo ulikuwa wa mwisho wa ligi kwa Azam mwaka 2022.

Chanzo: Mwanaspoti