Azam FC imeanza usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao na tayari imewatambulisha mastaa wapya wanne, wakiwamo wawili kutoka Colombia na Mali, lakini haijaishia hapo kwani ipo hatua za mwisho kunasa saini ya aliyekuwa mshambuliaji wa Mashujaa, Adam Adam.
Hadi sasa Azam imewatambulisha Wacolombia, Ever Meza (kiungo) na Jhonier Branco (mshambuliaji) sambamba na beki Mamadou Diaby na kiungo Frank Tiesse wote raia wa Mali na sasa huenda anayefuata kutambulishwa akawa Adam.
Taarifa ambazo zimethibitisha ni kuwepo kwa mazungumzo ya kimkataba kati ya Azam na Adam ambaye ni mchezaji huru baada ya kumaliza muda wake ndani ya Mashujaa aliyoichezea kwa msimu uliopita na kuibuka mfungaji bora wa kikosi hicho akipachika jumla ya mabao saba.
Taarifa za ndani zinaeleza dili la Adam na Azam lipo katika hatua za mwisho kukamilika kwani tayari pande zote mbili zimekubaliana kila kitu hivyo kilichobaki ni staa huyo aliyewahi kuzichezea African Lyon, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Polisi Tanzania, JKT Tanzania na Etihad Tripol na Allwahda za Libya kumwaga wino kwa matajiri hao wa Chamazi.
Moja ya vigogo wa Azam alitudokeza uwepo wa dili hilo na kuweka wazi kila kitu kitakamilika baada ya timu hiyo kurejea Dar es Salaam ikitoka Unguja ilikoenda kwa ajili ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), dhidi ya Yanga.
“Tunamsajili Adam, kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha akiwa na Mashujaa, hasa tunazingatia matakwa ya kocha, hivyo timu ikirudi kutoka Zanzibar anaweza akatangazwa muda wowote,” alisema kiongozi huyo aliyeomba jina lake lisitajwe na kuongeza;
“Ni vitu vichache vimebakia kukamilisha dili lake, ndio maana nashindwa kusema moja kwa moja tumemalizana naye ila ninachojua kama mambo yasipobadilika basi msimu ujao tutakuwa naye.”
Alipotafutwa Adam kuzungumzia uhamisho wake kwenda Azam alisema kwa sasa ni mchezaji huru hivyo hizo ni tetesi tu ila yupo tayari kuongea na timu yeyote itakayomuhitaji.
“Itakuwa ni tetesi tu kwa kuwa niko huru, ila kwa kuwa ni mchezaji nipo tayari kucheza timu yeyote ambayo tutafika makubaliano.