Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam kujichimbia Zanzibar

Azam FC Na Coaches Azam FC

Sat, 20 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Azam kinarejea mazoezini rasmi kesho kwa lengo la kuendelea na programu mbalimbali za kujiweka fiti kwa ajili ya mashindano mbalimbali huku kikitarajia kwenda visiwani Zanzibar Januari 25 ili kuweka kambi ya takribani wiki mbili.

Timu hiyo ambayo awali ilikuwa Zanzibar wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi itarudi tena visiwani humo huku Kocha Mkuu, Youssouph Dabo akisema ni sehemu tulivu ambayo itawajenga wachezaji kushika mbinu haraka kabla ya kurejea Bara.

"Tuna sehemu nyingi ambazo tumependekeza ila kubwa ni kuweka kambi Zanzibar katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama, lengo kubwa ni kuhakikisha tunajiandaa vizuri ili tutakaporudi katika ushindani tuwe tayari kupambana," alisema Dabo.

Kuhusu usajili wa timu hiyo, Dabo alisema amefurahishwa kwa kiasi kikubwa na nyota wapya kwani hakutaka maingizo mengi mapya isipokuwa alilenga nafasi zenye mapungufu ndizo zifanyiwe kazi na anawashukuru viongozi kwa kuweza kufanikisha.

Nyota wapya waliosajiliwa ni, Mohamed Mustafa aliyetokea Al-Merrikh ya Sudan, beki wa kati, Yeison Fuentes kutoka timu ya Leones, mshambuliaji, Franklin Navarro kutokea Cortulua FC ya kwao Colombia na Adolf Bitegeko aliyetoka Volsungur IF ya Iceland.

Katika hatua nyingine makipa wawili wa timu hiyo, Abdulai Iddrisu na Ali Ahamada wameondolewa kwenye usajili baada ya kuonekana watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha mbalimbali waliyoyapata mwaka jana.

Iddrisu anauguza jeraha la bega lake la mkono wa kushoto alilofanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini sambamba na Ahamada anayesumbuliwa na goti la mguu wa kushoto huku akiondoka na kwenda Ufaransa kwa ajili ya uchunguzi wa matibabu zaidi.

***

Kocha Mkenya amkomalia Anuary

DAUDI ELIBAHATI

KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza amesema amemuandalia programu maalumu mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Anuary Jabir kwa lengo la kuhakikisha nyota huyo anarudi katika ubora wake tofauti na alivyouanza msimu akiwa na Kagera Sugar.

Nyota huyo aliyerejea Dodoma katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15 ameshindwa kuonyesha makali yake yaliyotarajiwa kwani hadi anaondoka Kagera hajafunga bao lolote la Ligi Kuu Bara jambo ambalo Baraza halihofii akiamini atamsaidia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema anatambua ubora wa mchezaji huyo na licha tu ya kutofanya vizuri alikotoka ila hiyo kwake hamsumbui kwani amemuandalia programu maalumu ikiwemo pia kumjenga kisaikolojia ili arudi katika ubora wake.

"Mchezaji yeyote anapitia katika kipindi kigumu ila inapofika katika wakati huo ni nafasi pia kama benchi la ufundi kuona ni kwa namna gani unamrudisha kwenye mstari, kwangu naamini atafanya vizuri hivyo sina mashaka kabisa," alisema.

Kwa upande wa Anuary alisema anajisikia furaha kurudi sehemu iliyompa jina huku akieleza kutofanya kwake vizuri akiwa na Kagera hadi sasa haina maana uwezo wake umeshuka isipokuwa ni jambo la kawaida ambalo linaweza kumtokea mchezaji yeyote.

Wakati akiitumikia Dodoma msimu wa 2021/2022, nyota huyo alimaliza akiwa amefunga jumla ya mabao saba ya Ligi Kuu Bara kisha akajiunga na kikosi cha Kagera Sugar ambapo msimu uliopita alimaliza na mabao matano ingawa hadi sasa hajafunga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live