Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam ilivyobeba ndoo kibabe Rwanda

Azam Fc Pict Azam ilivyobeba ndoo kibabe Rwanda

Mon, 5 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC imeendelea kukunjua makucha baada ya juzi usiku kupata ushindi wa bao 1-0 na kubeba ubingwa ikiwa jijini Kigali, Rwanda.

Ndiyo, kama ambavyo Simba ilivyokuwa Kwa Mkapa kuhitimisha tamasha la Simba Day na kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda au kama jana Yanga iliyokamilisha Wiki ya Mwananchi kwa kuvaana na Red Arrows ya Zambia, ndivyo Azam ilivyojimwambafai jijini Kigali katika kilele cha Tamasha la Rayon Sports Day la klabu ya Rayon Sports iliyopo Ligi Kuu ya Rwanda na kumaliza nafasi ya pili.

Tamasha hilo lililoambatana na mechi ya michuano maalumu ya kuwania Kombe la Choplife 2024, Azam haikulaza damu kwa kunyakua taji hilo kwenye Uwanja wa Kigali Pele.

Bao pekee lililowekwa wavuni kwa kichwa na Lusajo Mwaikenda katika dakika ya 57 akimaliza krosi ya Franck Tiesse ilitosha kuipa Azam taji hilo la kwanza kwa msimu mpya wa 2024-2025 ikiwa ugenini ikiichapa wenyeji Rayon Sports.

Azam inakuwa klabu ya pili ya Tanzania kwa hivi karibuni kubeba Kombe nje ya nchi, baada ya awali Yanga kutwaa Kombe la Toyota kwa kuicharaza wenyeji, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa mabao 4-0 mechi iliyopigwa wikiendi iliyopita nchini humo.

Katika tamasha hilo, wenyeji Rayon na Azam zilitumia kutambulisha vikosi vipya na jezi mpya, lakini kwa wageni iliitumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi ya ushiriki wa michuano ya Ngao ya Jamii na Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Azam iliyoanza kambi ya maandalizi ya msimu mpya tangu mapema Julai ikianzia Chamazi, Dar es Salaam kisha kwenda Zanzibar na kucheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Zimamoto na kushinda mabao 4-0, ilienda Morocco kuweka kambi ya zaidi ya wiki mbili na kucheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa.

Ilianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya US Yacoub Mansour, kisha ikatoka sare ya 1-1 Union Touarga kabla ya kulala 4-1 mbele ya mabingwa wa zamani wa Morocco na Afrika, Wydad Casablanca ndipo ikaenda Rwanda kushiriki tamasha hilo na kupata ushindi huo na kutwaa kombe hilo la ChopLife.

Katika mchezo huo wa juzi jijini Kigali, Azam iliungana na klabu za Simba na Yanga zilizofanya matamasha ya Simba Day na Wiki yas Mwananchi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kutesti nyota wapya wa kikosi hicho kwa ajili ya michuano inayokabiliana nayo ikiwamo Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii mbali na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kuumana na APR ya Rwanda.

Kocha Youssouf Dabo na Bruno Ferry waliwaanika mashine mpya kama Franck Tiesse kutoka Mali na Mcolombia, Jhonier Blanco walioanza kikosi cha kwanza waliocheza vyema na kuisumbua ngome ya Rayon, timu inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' aliyerejea tena klabuni.

Mbali na nyota hao, Azam imewasajili pia Yoro Mamadou Diaby, Mamadou Samake na Cheickna Diakite wote kutoka Mali na Mcolombia Ever William Meza sambamba na mzawa Nassor Saadun, huku Evance Tepsie akirejesha kikosini kutoka KMC alikokuwa akicheza kwa mkopo.

Katika mchezo huo, Azam iliupiga mpira mwingi na kuonyesha msimu ujao mambo yatakuwa moto kutokana na mseto wa wachezaji waliopo wakiwamo waliokuwa msimu uliopita kama Feisal Salum 'Fei Toto', kipa Mohammed Mustafa aliyesajiliwa jumla kutoka Al Merrikh ya Sudan.

Wengine ni; Yannick Bangala, Yeison Fuentes Lusajo Mwaikenda,  Cheikh Sidibe, James Akaminko, Gibril Sillah, Adolph Mtasingwa, Nathaniel Chilambo, Pascal Msindo, Idd Seleman 'Nado', Abdallah Kheri 'Sebo', Zubeir Foba.

Kikosi hicho kilikuwa njiani kurejea nyumbani ili kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union, itakayopigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja, wakati Simba na Yanga zenyewe zikimalizana Kwa Mkapa siku hiyo hiyo na washindi wa mechi hizo kucheza fainali.

Mechi ya fainali itapigwa Jumapili ijayo mara baada ya mchezo wa kuwania nafasi ya tatu itakayozikutanisha timu zitakazopoteza mechi hizo za Alhamisi kisha Azam, Coastal na Yanga kugeukia mechi za kimataifa za CAF, Azam ikikaribisha APR, wakati Yanga itaumana na Vital'O ya Burundi zote zikicheza Ligi ya Mabingwa na Coastal itakuwa na kibarua mbele ya Bravo ya Angola katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Bila ya shaka kwa mechi ambazo timu hizo imezichezea zikiwa katika kambi za pre season nje ya nchi kisha kumalizia katika matamasha yaliyofanyika wikiendi iliyopita ni wazi vigogo na wawakilishi hao wa nchi wapio tayari kwa vita, Simba ikipangwa kucheza raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live