Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam, Mtibwa patachimbika Chamazi

Kagera Vs Azam U20 Azam, Mtibwa patachimbika Chamazi

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu ya Vijana U-20 imefikia patamu wakati leo mechi za nusu fainali zitakapopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, huku macho na masikio ya mashabiki yakiwa kwenye pambano la watetezi Mtibwa Sugar na Azam FC.

Mechi hiyo ya nusu fainali baina ya timu hizo zinazosifika kwa soka tamu kwenye ligi hiyo iliyoanza Juni 21, itapigwa kuanzia saa 12:00 jioni mara baada ya pambano la nusu fainali ya kwanza baina ya Kagera Sugar na Geita Gold.

Katika pambano la juzi usiku, Azam ilikamilisha timu za kucheza hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuifumua Tanzania Prisons kwa mabao 3-1 katika mechi kali ya robo fainali iliyopigwa uwanjani hapo na kuzifuata Mtibwa, Geita Gold na Kagera Sugar zilizotangulia mapema.

Azam ilipata ushindi kupitia mabao ya Ashrafu Kibeku, George Chande na Abdulkarimu Kiswanya, huku bao pekee la kufutia machozi ya Prisons likifungwa na Idd Kichindo na leo itavaana na Mtibwa Sugar inayoshikilia taji hilo kwa misimu minne mfululizo.

Mtibwa ilitinga nusu fainali baada ya kuinyoosha Coastal Union kwa mabao 2-0 kupitia Athuman Makambo na Said Salum na kabla ya pambano baina ya timu hizo zilizojizolea mashabiki wengi, mapema saa 9:00, alasiri Kagera Sugar itapepetuana na Geita Gold.

Kagera ilipenya hatua hiyo kwa kuifumua Dodoma Jiji kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Said Said na Kasimu Faki, ilihali Geita iliiduwaza Mbeya City kwa kupindua meza jioni ilipoinyuka mabao 2-1.

Mbeya City iliongoza kwa muda mrefu mchezo huo mkali kwa bao la dakika 19 lililofungwa naBaraka Mwalibunju na wakati ikiamini imevuka kwenye nusu fainali, Geita ilitumia dakika nne za nyongeza za mchezo huo kufunga mabao mawili kupitia Nicodemas Ntarema na Shija Abdallah.

Ligi hiyo iliyoanza kuchezwa kwa makundi ilishirikilisha jumla ya timu 16, huku vigogo Simba na Yanga zikimaliza mkiani mwa makundi yao kama ilivyokuwa kwa Namungo na Singida Big Stars.

Chanzo: Mwanaspoti