Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam, Mtibwa mechi ya kisasi

Azam FC Vs Zimamoto Azam, Mtibwa mechi ya kisasi

Sun, 7 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uhondo wa mechi za hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho unaendelea leo kwa pambano linalowakutanisha mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, Azam FC itakayoikaribisha Mtibwa Sugar katika mechi ya kisasi itakayopigwa usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Timu hizo zitavaana kuanzia saa 3:00 usiku ili kusaka tiketi ya kwenda robo fainali kuungana na Namungo, Tabora United, Geita Gold na Coastal Union zilizotangulia mapema na jana ilipigwa mechi nyingine kati ya KMC na Ihefu. Mtibwa inakutana na Azam ikiwa na kumbukumbu ya kutoka kupasuliwa mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Novemba 24, mwaka jana, lakini ikiwa haijawahi kuitambia Azam tangu Julai, 2020 hivyo mechi ya leo itakuwa ni nafasi yao ya kulipa kisasi dhidi ya wenyeji wao hao.

Katika mechi sita mfululizo ambazo timu hizo zimekutana katika Ligi Kuu tangu 2021, Azam imeshinda mara zote, huku kocha wa Mtibwa, Zubeir Katwila alikaririwa watashuka uwanjani leo kwa nia moja ya kujivua unyonge mbele ya wapinzani wao hao.

Mtibwa ni mabingwa wa michuano hiyo kwa msimu wa 2018 msimu mmoja kabla ya Azam kulibeba 2019, ikiwa na maana mechi hiyo ni pambano la mabingwa wa zamani, lakini kila mmoja akiwa na kiu ya kutinga robo fainali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Azam, Youssouf Dabo alisema kikosi hicho kipo kamili tayari kwa mchezo huo ambao ameutaja ni muhimu kwao kusaka nafasi ya kuendelea hatua inayofuata.

Dabo alisema malengo yao ni kuona kwamba wanapata ushindi kwenye mchezo huo ili kuweza kutimiza jambo lao la kusonga hatua inayofuata na hatimaye kutwaa ubingwa.

“Tupo imara na tunahitaji kurejea katika mashindano ya kimataifa, ili uweze kurudi huko ni lazima upate ushindi usonge hatua nyingine na kutwaa taji tunaamini tutafanya vizuri, mashabiki watupe sapoti,” alisema Dabo na kuongeza;

“Tunawaheshimu wapinzani wetu tutakutana nao wao wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa ligi dhidi yetu tukiwafunga mbao 5-0 hiyo haiwezi kutufanya tukajisahau tumejiandaa kwenda kushindana na wachezaji wapo kwenye hali nzuri.”

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema wataingia kwenye mchezo huo kwa ajili ya kwenda kusaka matokeo huku wakiwaheshimu wapinzani wao.

“Hautakuwa mchezo rahisi lakini tumejiandaa kwaajili ya kushindana lengo ni kuona tunapata matokeo na kusonga hatua inayofuata.”

Mara baada ya mechi hiyo ya sita ya 16 Bora, zitasaliwa michezo miwili ya kukamilisha ratiba kwa vigogo Simba na Yanga kucheza kesho na keshokutwa ugenini.

Yanga ambayo ni watetezi itakuwa Jamhuri, Dodoma kuumana na wenyeji wao Dodoma Jiji na Simba itakuwa Lake Tanganyika, Kigoma dhidi ya Mashujaa.

Chanzo: Mwanaspoti