Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam, Kagera balaa lipo hapa

Juma Mgunda Sababu.jpeg Azam, Kagera balaa lipo hapa

Sat, 25 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Macho na masikio ya mashabiki wa Ligi Kuu Bara yanaelekezwa kwenye viwanja viwili leo ikiwa ni katika mchezo kati ya Azam FC ambayo itakuwa nyumbani ikivaana na Kagera Sugar na Simba itakayovaana na KMC jijini Arusha.

Ni mechi ambazo zitaamua hatima ya timu gani itakomaa  kwenye nafasi ya pili kutokana na Azam na Simba  kulingana pointi tofauti ikiwa ni mabao ya kufungwa, ambapo matajiri wa Jiji la Dar es Salaam wamefungwa 20 ilhali Mnyama akifungwa 25. Timu hizo kila moja imefunga mabao 56.

Achana na ubingwa ambao tayari Yanga iliutwaa ikiwa na michezo mitatu mkononi, vita iliyopo sasa ni nafasi ya pili ambayo inashikiliwa na Azam baada ya kukusanya pointi 63 sawa na Simba iliyo nafasi ya tatu.

Timu hizo zitakuwa kibaruani, ambapo Azam itakuwa Uwanja wa Azam Complex kuikabili Kagera iliyo nafasi ya tisa baada ya kukusanya alama 31 kwenye michezo 28.

Azam na Kagera zimekutana mara 27 kuanzia Septemba 15, 2010 na katika michezo hiyo, Wanalambalamba ndio kinara, ikishinda mechi nyingi na katika michezo mitano ya karibuni wageni hao wameshinda miwili, huku wenyeji wakishinda mmoja na sare mbili.

Mtanange wa timu hizo kusaka pointi tatu utakuwa mkali kutokana na kila timu kuzihitaji ili kujihakikishia mazingira mazuri kwenye msimamo na ndio unafanya mchezo huo kutoa picha ya kuwa bora na wa ushindani.

Kagera ndio timu mwenyeji atakuwa na kibarua kigumu zaidi ya Azam ambayo inasaka pointi ili kuendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

Vita hiyo endapo Azam itashinda itaendelea kusalia katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 66, ikiizidi Simba ambayo pia endapo itapata matokeo mazuri dhidi ya KMC itafikisha alama hizo.

Kagera inatakiwa kushinda mchezo huo ikizingatia iko nyumbani na endapo itavuna pointi tatu itazishusha Namungo, Ihefu FC na Tanzania Prisons kwani itafikisha pointi 34 na kupaa hadi nafasi ya sita.

Timu hizo mbili katika mechi tano zilizopita, Azam inaonekana kuwa na ubora kutokana na kushinda mechi nne ikipoteza moja, huku Kagera imefungwa mechi mbili na kuambulia sare tatu.

Ukuta wa Kagera Sugar utakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha unawalinda mastaa wa Azam FC, hasa eneo la ushambuliaji wakiongozwa na kinara wa ufungaji wa timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' kutokana na kuwa kwenye kiwango bora akitumia nafasi katika kila mchezo anaoupata.

Fei Toto mwenye mabao 16 amekuwa bora eneo lake asipofunga, basi atatengeneza pasi itakayozaa bao, na hadi sasa katoa pasi saba ambazo ziliisaidia Azam FC kupata mabao.

MINZIRO vs DABO

Vita nyingine ni mbinu bora kwa wapinzani hao kwenye mchezo huo kwani dakika 90 nje ya mapambano ya wachezaji kiwanjani zinaamuliwa na mipango bora ya makocha.

Kocha Freddy Felix 'Minziro' amesema anawaheshimu Azam na anatambua maeneo bora na madhaifu yao amekaa na wachezaji wake kuhakikisha anawahimiza wafanye vitu sahii ili waweze kupata matokeo.

"Tunakutana na timu ambayo imeimarika na ina ubora maeneo mengi tutaingia kwa kuwaheshimu huku tukiwa tumeandaa mbinu sahihi zitakazotupa matokeo yatakayotuweka sehemu nzuri kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao,"  alisema Minziro beki wa kushoto wa zamani wa Polisi Zanzibar na Yanga.

Youssouf  Dabo, kocha wa Azam alisema wanatambua umuhimu wa mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar leo wamefanya kila kitu kuhakikisha wanaibuka na matokeo yatakayoendelea kuwaweka nafasi ya pili.

"Tunahitaji kufunga mabao mengi na kushinda ili kujitengenezea mazingira mazuri kwenye msimamo wanaotukimbiza tofauti yetu na wao ni idadi ya mabao hivyo tunataka mabao na pointi dhidi ya Kagera Sugar."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live