Kikosi cha Azam FC kimewasili salama nchini Benghazi-Libya kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya wenyeji wao Al Akhdar.
Azam FC kesho Jumamosi (Oktoba 08) itashuka katika dimba Omar Al-Mukhtar majira ya saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, ikiwa na matumaini ya kupambana na kupata ushindi ugenini, kabla ya kurudi nyumbani kwa mchezo wa Mkondo wa Pili.
Kabla ya kuondoka nchini jana Alhamis (Oktoba 06), Kocha Mkuu wa Azam FC Denis Lavagne alisema kazi kubwa wanayokwenda kuifanya Libya ni kupambana ili kupata matokeo, ambayo anaamini yatakisaidia kikosi chake kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mwishoni mwa juma lijalo Azam Complex-Chamazi, Dar es salaam.
Kocha huyo aliyewahi kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008 akiinoa Cotton Sports ya Cameroon na 2021 alipoifikisha JS Kabaiyle ya Algeria fainali ya Kombe la Shirikisho alieleza kulijua vyema soka la Afrika na kuwasoma Al Akhdar, hivyo atatumia uzoefu wake kwenye mchezo wa Jumamosi (Oktoba 08).
“Tutahakikisha tunapambana ugenini dhidi ya wenyeji wetu Al Akhdar, najua mchezo hautakua rahisi kwa sababu soka la Afrika limegubikwa na mambo mengi ya ndani na nje ya Uwanja, lakini kazi inayotupeleka Libya ni kupambana na kupata matokeo.”
“Naamini mambo yakitunyookea ugenini, tukirudi hapa tutakuwa na nafasi nzuri ya kumalizia pale tutakapoishia ugenini, nimewaandaa vizuri wachezaji wangu kuelekea mchezo wetu dhidi ya Al Akhdar, nasisitiza tutapambana na kupata matokeo ugenini.” alisema kocha huyo