Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC yasalia Zenji licha ya kufurushwa Mapinduzi Cup

Azam Namungo Azam FC

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kikosi cha Azam FC kimeendelea kuweka kambi yake visiwani hapa kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa Januari 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Wachezaji wa Azam jana asubuhi walianza programu ya mazoezi ya gym baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya Singida Big Stars kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali.

Akizungumza nasi jana, Kocha Mkuu wa Azam FC, Kally Ongala, alisema sasa hivi wanatumia muda walionao kujiweka tayari kuwakabili Prisons na baadaye kushusha kikosi imara kwenye mechi ya Kombe la FA.

Kally alisema wameamua kubakia Zanzibar ili kupata nafasi sahihi ya kurekebisha mapungufu waliyoyabaini kabla ya kurejea Dar es Salaam kuendelea na mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tumeona tuendelee kubakia Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi, tunatarajia kucheza mechi za kirafiki na timu za hapa, ili kumpa nafasi kipa wetu mpya, Abdulai Iddrisu, aliyesajiliwa hivi karibuni,” alisema Kally.

Kocha huyo aliongeza wamejiondoa katika vita vya ubingwa lakini mipango yao mikubwa ni kuhakikisha wanafanikiwa kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu na kutwaa Kombe la Shirikisho.

“Kufikia malengo hayo ni lazima tufanye maandalizi mazuri, kufanyia kazi madhaifu ya kikosi chetu na wachezaji wanafanya yale tunayowaelekeza katika uwanja wa mazoezi na kuhamishia kwenye mechi kwa kutafuta matokeo ya ushindi,” alisema kocha huyo.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC iko katika nafasi ya tatu nyuma ya vinara na mabingwa watetezi, Yanga na Simba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live