Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo siku ya Jumamosi itakuwa kibaruani kutetea taji lake la Kombe Mapinduzi, pale itakapokuwa ikipambana na URA ya Uganda kwenye mchezo wa fainali utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15 usiku.
Mbali na kuwa mtihani wa kutetea ubingwa walioutwaa mwaka jana kwa kuifunga Simba bao 1-0, Azam FC pia itakuwa ikifukuzia rekodi mbili na kuweka historia mpya kwenye michuano hiyo iliyoshirikisha timu 11 mwaka huu.
Rekodi ya kwanza ni ile ya kurudia mafanikio waliyoyapata miaka mitano iliyopita walipolitwaa taji hilo mara mbili mfululizo mwaka 2012 na 2013, hivyo wakilibeba tena leo itakuwa wamerudia mafanikio hayo kwani mwaka jana walilitwaa na mwaka huu pia.
Mpaka sasa michuano hiyo ikiwa katika mwaka wa 11, hakuna timu yoyote iliyolitwaa taji hilo mara mbili mfululizo isipokuwa Azam FC iliyoweza kufanya hivyo.
Rekodi ya pili, Azam FC ikilitwaa taji hilo leo kihistoria itakuwa ndio timu pekee iliyolitwaa mara nyingi miongoni mwa timu zilizowahi kubeba kombe hilo, itakuwa imefanya hivyo mara nne na kuizidi Simba ambayo imelitwaa mara tatu.
Azam FC imetinga fainali baada ya kuichapa Singida United bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji, Shaaban Idd, huku URA ikiitoa Yanga kwenye hatua ya nusu fainali kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3 baada ya suluhu ndani ya dakika 90.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya mwisho hapo jana jioni, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema tayari wamemaliza kazi ya maandalizi ya mchezo huo huku akidai wachezaji wako kwenye hali nzuri tayari kufanikisha ushindi muhimu kesho.
“Mara nyingi unapocheza na timu ngumu unatengeneza mipango yako lakini inakuwa ni siri ya klabu kwa hiyo hatuwezi kusema tunaingia na mbinu gani lakini URA tumeshacheza nao zaidi ya mara moja na tunawajua, tumewaona walivyokuwa wakicheza mechi za hapa na tunajipanga ni jinsi gani tutavunja nguvu zao na kutumia udhaifu wao,” alisema Idd Cheche.
Cheche ameongeza timu hiyo kadiri inavyoendelea kucheza mechi za michuano hiyo wanazidi kuimarika akidai kuwa walivyoanza kucheza mechi za mwanzo ni tofauti na wanavyomalizia.
“Kwanza tunavijana wengi na wote wako tayari kwa hiyo wanatupa hamasa kiasi kwamba kadiri unavyokwenda hawaonyeshi kuchoka na wanaonyesha kupambana zaidi na kiwango kinazidi kuongezeka kwa hiyo inatupa matumaini kutetea kombe letu,” alisema.
Akielezea siri ya mafanikio ya kikosi hicho kuingia fainali mbili mfululizo, Cheche aliongeza kuwa: “Siri ya mafanikio ni umoja na kukubaliana, wote tunaumoja, tumekubaliana hii ni kazi yetu tuhakikishe tunaifanya vizuri na tunaimalizia vizuri.”
Naye Nahodha wa timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema kuwa: “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kambi yetu iko vizuri, wachezaji wote wako kwenye hali nzuri kila mtu nafikiri anatamani kupata nafasi ya kuiwakilisha Azam FC na kuipatia matokeo.”
Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, wakitwaa taji hilo watakuwa wamebeba kombe la kwanza msimu huu huku wakiwa kwenye hatua nzuri ya kuyatwaa mengine mawili, lile la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) wakiwa wamelingana pointi na Simba kileleni kila mmoja akiwa nazo 26.
Katika hatua nyingine, pia Azam FC imetinga raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) ikitarajia kukipiga na Shupavu FC ya Morogoro kati ya Januari 31 au Februari Mosi mwaka huu, mchezo ukipigwa ugenini Kilombero, Morogoro.