Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC yabanwa mbavu na Tabora United

Azam FC Dubeeeeeee Azam FC yabanwa mbavu na Tabora United

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Azam FC imesogea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa suluhu na Tabora United.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, imeifanya Azam kushika nafasi ya pili na pointi 36, sawa na Simba japo kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam kimezidi mchezo mmoja na kinaongoza kwa mabao ya kufunga.

Mchezo huo ni wa 16 kwa Azam ambapo kati ya hiyo imeshinda 11, sare mitatu na kupoteza miwili huku kwa upande wa Tabora ikisalia nafasi ya 13 katika msimamo na pointi zake 17 baada ya kushinda mitatu, sare minane na  kupoteza mitano.

Mchezo huu ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kutokana na kilichotokea mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Agosti 16, mwaka jana ambapo Tabora ilifungwa mabao 4-0, huku mechi hiyo ikichezwa dakika 18 tu tofauti na ilivyokuwa kawaida 90.

Sababu za mchezo huo kuchezwa dakika hizo ni kutokana na kitendo cha wachezaji wengi wa Tabora kutokuwa na vibali na kuanza wanane pekee uwanjani na baada ya wengine wawili kuumia na kubaki sita mechi hiyo ilishindwa kuendelea kwani kanuni za soka haziruhusu.

Matokeo hayo yanaifanya Tabora kufikisha michezo sita mfululizo bila ya ushindi tangu mara ya mwisho iliposhinda mabao 2-1, dhidi ya Mtibwa Sugar, Desemba Mosi mwaka jana huku kwa upande wa Azam imefikisha mechi ya tisa mfululizo bila kupoteza.

Mchezo mwingine, Geita Gold ilijikuta ikipoteza nyumbani Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita baada ya kufungwa mabao 2-1, dhidi ya Ihefu ikiwa ni kichapo cha pili mfululizo baada ya mechi iliyopita kulala 2-1, mbele ya Azam FC.

Mabao ya Ihefu katika mchezo huo, yalifungwa na nyota wapya wa kikosi hicho, Elvis Rupia na Marouf Tchakei huku lile la kufutia machozi likifungwa na Tariq Seif.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live