Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC wasubiriwa kwa hasira Manungu

Azam FC Kali Ongala Benchi la Ufundi la Azam FC

Thu, 10 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huko Mtibwa Sugar unaambiwa tayari wamesahau kipigo kizito walichopata mbele ya Simba na sasa wanakusanya nguvu kuhakikisha hasira zote zinaishia kwa Azam FC watakapokutana uwanjani.

Mtibwa Sugar ikicheza Uwanja wa Mkapa dhidi ya Simba, walikumbana na mvua ya mabao 5-0 na sasa watakuwa nyumbani Manungu kuwakaribisha Azam mchezo utakaopigwa Novemba 12.

Azam inawakabili Wakata Miwa hao ikikumbuka ushindi wa mchezo wao wa jana ikiwaadhibu Dodoma jiji bao 2-1 na kukaa nafasi ya pili kwa pointi 20, huku wapinzani wakiwa na alama 15 nafasi ya saba.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Awadh Juma alisema kwa sasa wanaendelea kurekebisha makosa yalioonekana lakini matokeo hayo walishasahau na wanajiandaa na mechi ijayo na Azam.

Alisema ligi ni ngumu na wanafahamu mechi hiyo itakuwa na upinzani mkali kutokana na Azam walivyo hivi sasa na kwamba wanaamini kwa maandalizi waliyonayo watapata ushindi.

“Ni mechi nyingine ngumu kwa sababu Azam wamekuwa na mwenendo mzuri kwa mechi zao za karibuni, ishu ya kufungwa mabao matano tumeshasahau na tunajipanga upya na mechi ijayo,” alisema Juma.

Kipa wa timu hiyo, Hamad Kaded alisema anaamini idadi ya mabao aliyofunga haitajirudia tena iwapo atapata nafasi na kwamba watawaheshimu wapinzani na kucheza kwa umakini na tahadhari ili yasijitokeze mengine mazito.

“Nafikiri makosa yaliyoonekana makocha waliona, lakini hata sisi wachezaji tuliumizwa na matokeo yale, tunaamini mchezo na Azam tunawapa raha mashabiki,”alisema Kipa huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live