Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC wanaitaka ndoo ya Ligi Kuu

Azam Kuendelea Na Mwendo Wa 5 0 Leo Azam FC wanaitaka ndoo ya Ligi Kuu

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ushindi mara tano mfululizo ilioupata Azam FC na kukaa kileleni kwenye Ligi Kuu Bara umewanogea wakali hao wa Chamazi na sasa wameanza kuwaza ubingwa.

Azam ilianza kushinda Novemba Mosi ilipoichapa Mashujaa mabao 3-0, kisha ikaifuata Ihefu na kuifunga 3-1, baada ya hapo ikarejea Dar es Salaam na kuifumua Mtibwa Sugar 5-0, dozi ambayo baadaye iliitoa tena kwa KMC na juzi ikaifunga JKT Tanzania 2-1.

Kocha wa timu hiyo, Msenegali Youssouf Dabo alisema matokeo hayo yamerejesha morali kikosini na sasa wanawaza kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo.

“Ni furaha kwangu kuona wachezaji wanafanya kile tunachokubaliana. Nawapongeza kwa hilo na kiukweli morali imekuwa ya hali ya juu kikosini,” alisema Dabo.

“Tunataka kuendelea kufanya hivi katika mechi zijazo na baada ya hapo ndio tutajua nini kinakwenda kutokea kuhusu ubingwa.”

Akizungumzia mafanikio ya timu hiyo, kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema Azam ilikosea kwenye mechi za kwanza, lakini kiwango inachokionyesha kwa sasa inaweza kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa msimu huu.

“Timu iko vizuri na inaonekana kuamka lakini shida ilipoteza baadhi ya alama muhimu katika mechi za mwanzo. Ukiangalia msimamo ulivyo wako kileleni, lakini Simba na Yanga zikicheza na kushinda mechi zao basi Azam inashuka,” alisema Mwaisabula.

“Kwa sasa ni mapema kuwawekea dhamana ya ubingwa, lakini mpira huwa una matokeo ya kushangaza. Tusubiri tuone mwisho itakuwaje.”

Azam ipo kileleni mwa msimamo wa ligi na alama 28 baada ya mechi 12 ikiwa imeshinda tisa, sare moja na kupoteza mbili ikifunga mabao 31 yakiwa ni mengi zaidi kwenye ligi hadi sasa na kuruhusu 10 ambapo mechi ijayo itacheza na Kagera Sugar ugenini, Desemba 21.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: