Matajiri wa Chamazi, Azam FC wapo katika kiwango bora sana. majuzi wameichapa Kagera Sugar mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. Siyo tu ushindi, bali wamecheza katika kiwango bora.
Hiyo ni mechi ya sita mfululizo Azam FC inashinda baada ya kupoteza mara ya mwisho kwa Namungo FC. Tangu hapo wamekuwa kama mbogo aliyejeruhiwa. Hawashikiki. Hawakamatiki.
Wamefunga mabao 22 na kuruhusu mawili tu katika mechi hizo sita za mwisho. Wako moto kweli kweli.
Sasa unaweza kusema Azam FC inacheza kikubwa baada ya kupoteana wakati fulani. Huyo Kipre Junior ni kama ametiwa ndimu. Anacheza kwenye ubora wa juu.
Utulivu wake umeongezeka. Kasi yake imeongezeka. Uwezo wake wa kupiga chenga umeongezeka. Hakamatiki. Pen-gine huyu ndiye Kipre ambaye Azam FC walimuona na kumsajili. Hajawahi kuwa kwenye ubora wa juu kama ilivyo sasa tangu alipotua Chamazi.
Feisal Salum ‘Fei Toto’ amerejea katika ubora wake. Anaupiga mwingi. Anatoa pasi na kufunga. Kasi yake pia imeongezeka. Ndiyo ubora ambao Azam FC waliutaka kutoka kwake.
Uzuri ni kwamba Azam FC sasa inaonyesha ukubwa wa kikosi chake. Akikosekana fulani, anayekuwepo anaonyesha ubora pia. Akitoka mtu, anayeingia naye anakwenda kuupiga mwingi. Ndiyo kama ilivyo kwa Iddi Nado. Amekuwa ‘Super sub’. Karibu kila mechi anayoingia anaonyesha kitu cha tofuati.
Hivi ndivyo timu kubwa inapaswa kucheza. Inatakiwa kuogopwa na timu ndogo. Ndiyo kama sasa, kila timu inaogopa kukutana na Azam FC katika zama hizi.