Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC ni timu ya mchongo tu

Azam FC Michongo Kikosi cha Azam FC

Mon, 24 Jan 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Azam FC. Timu iliyotabiriwa kuwa mkombozi wa soka la Tanzania. Timu ya Familia ya Bilionea, Salim Said Bakhersa. Timu iliyopewa nafasi ya kuzipa changamoto Simba na Yanga. Nini kimetokea?

Ni swali ambao watu wengi wanajiuliza sana kwa sasa. Azam FC imepoteza dira. Imekuwa timu ya kawaida kama Kagera Sugar ama Ruvu Shooting.

Siyo timu inayotisha tena. Mechi zake hazisisimui tena. Kitu kizuri pekee kilichosalia kwa Azam FC ni ule uwekezaji wao pale Chamazi pamoja na basi lao jipya la Mercedes Benz.

Inashangaza sana. Lakini ni kitu gani hasa kimeikumba Azam FC? Kwa miaka minne sasa imeshindwa kushindania ubingwa wa Tanzania. Imeshindwa kumaliza katika nafasi mbili za juu kama ilivyokuwa ikifanya zamani.

Msimu wao wa mwisho kufanya vizuri ilikuwa 2015/16. Ni msimu huo ikiwa chini ya Sterwart Hall iliweza kukimbizana na Yanga hadi dakika za mwisho. Zama hizi Azam FC inatoka kwenye mbio za ubingwa mapema tu kabla hata msimu haujafika nusu. Ni ajabu na kweli.

Leo acha nikueleze mambo machache kuhusu Azam FC. Tuanze na uongozi wa timu hiyo - waliopo wanatosha katika nafasi zao?

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ anatosha katika nafasi hiyo? Sidhani. Ni mtendaji mkuu wa kawaida tu.

Kwanza, kazi yake kubwa iko kwenye Kiwanda cha Unga pale Mzizima. Akiamka asubuhi anapambana kwanza na shughuli za unga. Anapambana na mahesabu ya unga pale Mzizima. Kisha baadaye ndio aanze masuala ya soka. Uliona wapi hili huko duniani?

Popat ana uwezo mkubwa wa kucheza mpira, lakini siyo kiongozi mzuri wa soka. Katika nyakati zake, Azam FC imefanya usajili mwingi wa ovyo. Timu hiyo imekuwa ikiokota wachezaji wa kawaida na kuwaleta pale Chamazi - wanacheza kwa miezi kadhaa na kutimka.

Wamekuja wengi sana. Ni ngumu kuwataja wote. Kina Ditram Nchimbi, Ally Niyonzima, Akono Akono na wengineo. Timu haifanyi utafiti mzuri kabla ya kusajili wachezaji. Matokeo yake wanachota pesa za bure pale Chamazi kisha wanaachwa.

Pili, Azam FC imeshindwa kupata kocha wa maana chini ya Popat. Ni mvivu kutafuta vitu vipya. Katika nyakati zake, Aristica Cioaba alikwenda na kurudi. Wakamchukua Hans Van Pluijm na Juma Mwambusi waliowahi kuwa Yanga. Akaenda kumchukua George Lwandamina aliyewahi kuwa Yanga.

Ni kweli dunia haina makocha wapya? Inakuwaje Simba inapata makocha wapya wazuri kila siku, lakini Azam wanashindwa. Kocha mzuri kwa Azam FC ni yule aliyewahi kupita Yanga? Inachekesha sana.

Ajabu zaidi ni kwa hili lililotokea kwa Lwandamina. Mtu mmoja alitaka kuwapa Azam FC, Florent Ibenge. Kocha mkubwa Afrika. Lakini likakwamishwa dili hilo na kumleta Lwandamina. Nini kilitokea?

Katika nyakati za Popat Azam imewakosa wachezaji wengi mahiri kutokana tu na pengine uzembe. Mfano mzuri ni Khalid Aucho. Azam ilikuwa timu ya kwanza kuzungumza naye, lakini mwisho wa siku akaenda Yanga.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Rally Bwalya msimu uliopita. Azam ilikuwa ya kwanza kuzungumza na Bwalya, lakini mwisho wa siku akaenda Simba. Hao ni baadhi tu wapo wengi zaidi waliokwenda Simba na Yanga licha ya Azam FC kuanza kuzungumza nao. Lakini, Azam ni timu inayomilikiwa na tajiri, ila inaishi kimasikini. Mpaka leo wachezaji wa Azam wanapata posho ndogo kuliko wachezaji wa Simba na Yanga. Sasa kuna faida gani ya kucheza kwenye timu ya tajiri kama hupati pesa? Posho za Azam ni nusu ya zile wanazopewa mastaa wa Simba.

Katika mashindano ya kimataifa posho ni ndogo zaidi. Mfano mzuri ni ule ugomvi uliotokea mwaka jana kati ya Sure Boy, Aggrey Morris, Mudathir Yahya na watendaji wengine wa timu. Ilikuwa inahusu Dola 20,000 za posho endapo wataitoa Horseed ya Somalia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Umewahi kufahamu Simba huwa inatoa posho kiasi gani kwenye mechi za kimataifa? Kwa mechi moja sio chini ya Dola 40,000 lakini Azam inatoa nusu yake. Na nusu hiyo wanapewa hadi watu wengine wa timu. Inashangaza.

Timu ya tajiri lazima iendeshwe kwa jeuri ya fedha. Inatakiwa kusajili wachezaji wakubwa kwa fedha nyingi. Inatakiwa kuchukua makocha wakubwa. Wachezaji wake wanapaswa kulipwa vizuri na kupewa posho za maana. Ndio maana halisi ya timu tajiri, lakini Azam inaendeshwa kimasikini.

Leo hii PSG, Manchester City, Chelsea ni timu za matajiri na unaona jeuri ya fedha katika timu hizo. Ndio maana kocha bora zaidi duniani Pep Guardiola yupo Man City, Lionel Messi yupo PSG. Ndio jeuri ya pesa, lakini Azam inasubiri Ibrahim Ajibu aachwe na Simba imsajili. Dunia haiishi maajabu.

Chanzo: Mwanaspoti