Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaendelea leo Jumatatu (Agosti 28) kwa mchezo mmoja utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex kati ya wenyeji Azam FC watakaoikaribisha Tanzania Prisons.
Azam FC wanaoshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi wanaingia na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kitayosce huku Tanzania Prisons wenyewe wakilazimisha sare ya bila kufungana na Singida Big Stars.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo, amesema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo ambao alisema anaamini utakuwa mgumu kutokana na kila timu kuhitaji pointi tatu.
Tunaingia kwenye mchezo huu tukiwaheshimu wapinzani wetu, tumeangalia mapungufu yetu kwenye michezo iliyopita na kuyafanyia kazi naamini, utakuwa mchezo mzuri kwa kila timu.
“Mchezo utakuwa mgumu licha ya kuwa tutakuwa nyumbani, tunaenda kucheza na timu nzuri yenye wachezaji wazuri , hivyo wataingia kwa lengo la kutafuta ushindi kama ambavyo nasi tutafanya,” amesema Dabo.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Fred Minziro alisema Azam FC wana kikosi bora chenye wachezaji wazuri na wenye uzoefu mkubwa ila amewaandaa vizuri wachezaji wake kwa mchezo huo.