Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC kuivaa Prisons Ligi ya U20

IMG 4470.jpeg Azam FC kuivaa Prisons Ligi ya U20

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Azam FC jana usiku imehitimisha mechi za makundi kwa kuifumua Simba kwa mabao 2-0 na kuifungasha virago kwenye Ligi Kuu ya Vijana U-20 inayoendelea katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na sasa washindi hao watavaana na Tanzania Prisons hatua ya robo fainali.

Azam imemaliza ikiwa kinara wa Kundi D ikikusanya jumla ya pointi 9 ikifuatiwa na Kagera Sugar iliyoifumua Ihefua kwa mabao 4-0 katika mechi ya mapema na sasa Wanalambalamba hao watavaana na wenzao wa Tanzania Prisons kwenye mechi ya robo fainali itakayopigwa kesho Jumatano.

Kwa kipigo hicho kilichotokana na mabao ya Daud Said na Cyprian Kachwele kimeifanya Simba kumaliza mkiani mwa kundi hilo kwa kukusanya pointi moja tuna kuunga na timu za Yanga, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting, Namungo, Ihefu, KMC na Singida Big Stars kuiaga ligi hiyo.

Mbali na mechi ya robo fainali kati ya Azam na Tanzania Prisons, michezo mingine ya hatua hiyo itazikutanisha Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya pili kwenye kundi D dhidi ya vinara wa Kundi B, Dodoma Jiji, huku watetezi Mtibwa Sugar iliyoibuka kinara wa Kundi A atakapovaana na Coastal Union iliyomaliza nafasi ya pili katika Kundi C.

Mechi nyingine ya mwisho ya hatua hiyo ya robo fainali itakutanisha kinara wa Kundi C, Geita Gold dhidi ya mshindi wa pili wa Kundi A, Mbeya City na washindi wa mechi hizo zitapenya hadi nusu fainali itakayopigwa Ijumaa hiii (Juni 30).

Mechi hizo za nusu fainali itazikutanisha mshindi wa mechi ya Mtibwa na Coastal atacheza na Azam au Prisons, ilihali mshindi wa Dodoma au Kagera ataumana na kati ya Geita au Mbeya City. Timu mbili zitakazopenya hapo kwa kushinda mechi hizo za nusu fainali zitaenda kukutana katika fainali itakayopigwa Julai 2, mechi itakayotanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ambao utazikutanisha zile zilizopoteza mechi za nusu fainali.

Mtibwa Sugar inalishikilia taji hilo kwa msimu wa nne mfululizo baada ya msimu uliopita kulitetea kwa kuifumua Mbeya Kwanza kwa mabao 4-1 katika mechi ya fainali kali iliyopigwa pia Azam Complex.

Ligi hiyo ya U-20 iliyoasisiwa mwaka 2018 kwa msimu huu ilianza kupigwa tangu Juni 21 ikishirikisha jumla ya timu 16 zilizopangwa nne nne katika makundi manne tofauti na kushuhudiwa vigogo Simba na Yanga zikishindwa kupata ushindi hata mmoja baada ya kila moja kupoteza mechi mbili na kuambulia sare moja tu na kuishia kuburuza mkia wa makundi hayo kama Singida BS na Namungo.

Hata hivyo, Singida na Namungo zimeiaga ligi hiyo kwa aibu kwa kushindwa kuambulia japo pointi moja kutokana na kila moja kupoteza mechi zote tatu za makundi yao

Chanzo: www.tanzaniaweb.live