Imefahamika kuwa Uongozi wa Azam FC hauna mpango wa kumwongezea mkataba kocha wake wa makipa, Dani Cadena baada tu ya msimu huu kuisha.
Cadena ambaye alijiunga na timu hiyo Juni 30, mwaka jana mkataba wake unaisha mwezi ujao (Juni) huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kumwongezea mwingine kutokana na kutokuwa chaguo la kocha mpya wa sasa Msenegali, Youssouph Dabo.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo ililiambia Mwanaspoti, Cadena sio chaguo la Dabo, hivyo mchakato wa kutafuta kocha wa makipa umeanza huku ikielezwa anataka kufanya kazi na mmoja wa marafiki zake.
“Kuna kocha mmoja ambaye amewahi kufanya naye kazi huko Senegal anataka kumleta hapa ila dili halijakamilika hadi sasa ingawa huo mchakato unaendelea kimya kimya kwa sababu Cadena sio chaguo la Dabo,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wa Cadena alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alikiri mkataba wake unaisha mwezi ujao ingawa hataki kuzungumzia zaidi hilo kwani akili yake bado ni kuitumikia Azam na wala sio vinginevyo.