Azam FC imeendelea kujifua kimyakimya kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikijiandaa na mechi ijayo ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, huku benchi likisisitiza litapiga kwenye mshono.
Katika mechi ya kwanza ya msimu huu, Azam iliitungua Simba bao 1-0 lililowekwa kimiani na Prince Dube na mechi ijayo ya marudiano itapigwa Februari 21 kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kocha wa kikosi hicho, Dani Cadena aliliambia Mwanaspoti wana muda mrefu wa kujiandaa wanaamini watafanya vizuri katika mechi ijayo.
Cadena alisema baada ya mechi na Dodoma iliyopigwa Februari 4, mwaka huu na kupoteza kwa mabao 2-1, waliwapa mapumziko mafupi wachezaji na sasa wamerejea ili kuanza rasmi maandalizi na mechi ya Simba.
“Tulipumzika kidogo na sasa tumereja uwanjani, tunafanya maandalizi makubwa ili tupate matokeo tunayoyataka katika mechi ijayo dhidi ya Simba,” alisema Cadena na kuongeza;
“Katikati hapo huenda tukacheza mechi moja au mbili za kawaida za kirafiki ili kupata tathmini ya tulichokifanya kabla ya kukutana na Simba.”
Pia, Cadena alifafanua juu ya mabadiliko ya kikosi cha kwanza kwa kusema; “Kila mchezaji wa Azam anahitaji kucheza na kwa bahati mbaya hauwezi kuwapanga wote kwenye mechi moja.
Wachezaji ambao wamekuwa wakiingia na kutoka kwenye kikosi cha Azam kwa sasa licha ya kuanza msimu vizuri ni, Tepsi Evance, Idriss Mbombo, Nathanael Chilambo, Isah Ndala, Pascal Msindo, Abdallah Sebo na Clephace Mkandala.