Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC iwekeze soka la wanawake

Amin Popat Azam FC iwekeze soka la wanawake

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Juni 15 mwaka huu, Azam FC ilitoa taarifa ya kufikia makubaliano ya ushirikiano wa mwaka mmoja na timu ya wanawake ya Fountain Gate Princess inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake Tanzania.

Lengo la kufikia makubaliano hayo ni kutimiza kanuni za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zinazolazimisha klabu shiriki kuwa na timu za wanawake ili zipate uhalali wa kushiriki.

Kanuni hizo zinafafanua klabu ambayo haina timu ya wanawake inapoteza hadhi ya kucheza ligi ya mabingwa Afrika, hivyo Azam FC imeamua kuungana na Fountain Gate ili isipoteze uhalali wa kucheza mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Hii sio mara ya kwanza kwa Azam FC kusaini makubaliano kama hayo kwani mwaka jana ilifanya hivyo kwa kuamua kushirikiana na Baobab Queens ya Dodoma kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Ni wazi Azam FC imefanya mambo makubwa na yenye maana kwenye soka hapa nchini lakini bado tunaidai iwekeze kikamilifu kwenye soka la wanawake ambalo limeanza kupiga hatua hivi sasa.

Hii ya kusaini mikataba ya muda mfupi mfupi na timu zinazoshiriki ligi ya wanawake kwa namna fulani inaifanya Azam FC kuonekana kama agenda ya soka la wanawake haina mpango nayo na inajilazimisha tu kusaini mikataba ya ushirikiano ya muda mfupi ili kuiridhisha CAF tu.

Kwa hadhi ambayo Azam FC inayo hivi sasa, inatakiwa kumiliki timu yake ya wanawake ambayo sio lazima ishiriki Ligi Kuu tofauti na sasa inafanya ilimradi tu ionekane imekidhi vigezo vya kikanuni lakini kiuhalisia haitamani kuwa na timu ya wanawake.

Huu ndio muda wa kuonyesha ukubwa kama ambavyo Yanga na Simba ambazo ni wakubwa wenzake waliamua kitambo kuwa na timu za wanawake.

Chanzo: Mwanaspoti