Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC iutazame upande huu muhimu

Azam Vs Art Solar 7 Azam FC iutazame upande huu muhimu

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Azam FC wamekuwa na mwanzo mzuri wa msimu wa Ligi Kuu unaozidi hata ule walikuwa mabingwa 2023/14.

Ushindi wa mechi nne na sare moja katika michezo mitano ya kwanza ni mwanzo mzuri unaozidiwa na misimu miwili tu katika historia ya klabu hiyo.

Msimu wa 2015/16 chini kocha Stewart Hall ambapo walishinda mechi zote tano, na msimu wa 2020/26 chini ya Aristica Cioaba ambao walishinda pia mechi zote. Msimu wa ubingwa, 2013/14, katika michezo mitano ya kwanza, Azam FC walishinda miwili na sare tatu.

Hata hivyo, Azam FC wangeweza kushinda mechi zote tano kama siyo makosa ya waamuzi, kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji walipokataliwa bao lao zuri.

Lakini zaidi ya mwanzo huu mzuri wa matokeo, Azam FC kwa upande mwingine imeanza vibaya sana kwa afya ya wachezaji wake.

Hadi raundi hii ya tano, Azam FC imezalisha majeruhi wanne wenye matatizo makubwa.

Abdallah Kheri Sebo ambaye atakuwa nje kwa zaidi ya miezi mitatu, baada ya kuumia kwenye mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.

Yahya Zaydi ambayo atakuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kuumia kwenye mchezo wa tatu wa ligi dhidi ya Singida Big Stars.

Prince Dube ambaye alitarajiwa kukaa nje kwa hadi wiki tatu baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Singida Big Stars. Hata hivyo alirejea mapema.

Na Yannick Bangala ambaye bado haijajulikana atakuwa nje kwa muda gani, aliyeumia katika mchezo wa nne dhidi ya Dodoma Jiji.

Huu ni mwanzo mbaya zaidi kwa Azam FC katika historia ya majeraha klabuni hapo. Mbaya zaidi wachezaji hawa wameumia bila kufanyiwa madhambi...yaani wameumia wakiwa wenyewe.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa zamani wa chama cha madaktari wa michezo (TASMA), Nassor Matuzya, aina hii ya majeraha pamoja na mambo mengine inatokana zaidi na suala zima la utimamu wa mwili.

1. Programu ya mazoezi 2. Kupasha moto mwili kabla ya mechi 3. Kupoza mwili baada ya mechi

Hapa ndipo inapokuja hoja ya andiko hili. Mtaalamu wa mambo yanayotajwa hapo pale Chamazi ni Mfaransa Jean Laurent Geronimi.

Kabla sijamjadili sana mtu huyu, ngoja niangazie kazi ya mtangulizi wake, Dk Moadh Hiraoui kutoka Tunisia.

Bwana huyu alitambulishwa na Azam FC wakati timu ikiwa Libya kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Akhdar.

Alikuja kuchukua nafasi ya Mhispaniola Mikel Guillen. Huyu jamaa alikuja mwanzoni mwa msimu huo na aliondoka baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao Azam FC walifungwa bao 1-0 jijini Mbeya.

Kwenye mchezo huo Azam FC ilipata majeruhi mmoja, Malickou Ndoye, ambaye alilazimika kukaa nje kwa miezi mitatu.

Huu ulikuwa mchezo wa tano wa ligi kwa Azam FC kwenye msimu. Baada ya hapo Azam FC ikapata majeruhi mmoja tu, Abdul Sopu ambaye hata hivyo hayakuwa majeraha mapya bali alijitonesha majeraha aliyoanza nayo tangu wakiwa El Gouna Misri kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Lakini zaidi ya hapo Azam FC haikuwa na majeruhi tena hadi mwisho wa msimu. Sasa ukipima hali hizi mbili halafu ukarejea kauli ya kitaaluma ya Dk Nassor Matuzya ndipo utabaini kwamba Azam FC ilipoteza mtu kwenye idara hii.

Hali kama hii iliwakuta Chelsea msimu wa 2015/16. Kuanzia 2011 hadi 2014 majeraha yalikuwa historia Stamford Bridge na chumba cha wagonjwa cha klabu kilikuwa tupu muda mwingi.  

Hali hiyo haikuja hivihivi tu bali ilitokana na kazi nzuri ya daktari wa wachezaji, Eva Carneiro.

Mwanadada huyu mrembo mzaliwa wa Gibraltar nchi inayogombaniwa na Hispania na Uingereza, alijiunga na Chelsea mwaka 2009 kama daktari wa wachezaji wa akiba kabla ya kupandishwa na kocha Andre Villas Boas mwaka 2011 kuwa daktari ya kikosi cha kwanza.

Katika wakati wake, wachezaji wa Chelsea walikuwa salama na klabu haikuwa ikiteseka kutibu wachezaji kama ilivyokuja kuwa baadaye.

Hiki ndicho kipindi ambacho ‘mzee mzima’ John Terry katika umri wa miaka 34, alicheza mechi zote 38 za Ligi Kuu, msimu wa 2014/15 na Chelsea kuwa bingwa.

Lakini siku ya kwanza ya msimu mpya wa 2015/16 kocha mkuu Jose Mourinho akagombana na dada huyo alipokwenda kumtibu Eden Hazard. Jambo likawa kubwa hadi akaacha kazi.

Kilichofuata baada ya hapo ni mfululizo wa majeraha klabuni Chelsea hadi ikawa kero. Huku ndiko inakoelekea Azam FC. Idadi ya majeruhi inaongezeka kwa kasi kulinganisha na msimu uliopita.

Majeraha ni kitu cha kawaida kwa wachezaji lakini katika mazingira kama haya ya Azam FC hali inatia shaka. Wachezaji wanatumia wenyewe tu, siyo kwa madhambi. Hii ni shida, tena shida kubwa sana.

Tofauti kidogo na Chelsea ni kwamba wachezaji wao walikuwa wanaumia kutokana na kufanyiwa madhambi hivyo kazi inakuwa moja kwa moja kwa daktari kwenye kuwafanya wawahi kurudi.

Lakini majeraha ya wachezaji kuumia wakiwa wenyewe maana yake kuna shida kwenye mazoezi siyo kwenye tiba... na hapo ndipo anapokuja bwana Jean Laurent Geronimi.

Hima Abdulkarim Popat liangalie tatizo hili. Timu yako imeanza vizuri msimu, lakini hadi raundi ya tano tayari ina majeruhi watano, kulikoni? Vipi msimu ukichanganganya?

Chanzo: www.tanzaniaweb.live