Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam FC inakosa 'ukorofi' wa kisoka

Azam Vs Art Solar 7 Azam FC inakosa 'ukorofi' wa kisoka

Tue, 26 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mpira licha ya kuwa ni mchezo wa kiungwana lakini unahitaji aina fulani hivi ya ukorofi ili mambo yaende.

Hapa ndipo unapokuja msemo maarufu wa kiingereza wa ‘take one for the team’ ambao maana yake ni kufanya kufanya jambo moja lisilo la kiungwana kwa faida ya timu.

Kwa mfano, wewe kama ni beki na mshambuliaji kakupita anakwenda kufunga, unaweza kumchezea madhambi na ukapata kadi nyekundu.

Hiyo kadi utakuwa umeipata kwa faida ya timu...ndiyo maana ya ‘take one for the team’.

Hii haishii tu kwa wachezaji uwanjani, inakwenda mbali zaidi hadi kwa viongozi.

Viongozi wa mpira hutakuwa kuwa na aina fulani ya ukorofi ili kuyafanya mambo ya taasisi wanayoiongoza, iwe klabu au chama, iende.

Sasa huo ndiyo ‘ukorofi’ wa kimpira, na ndiyo unaokosekana pale Azam Complex... siyo kwa wachezaji bali kwa viongozi.

Viongozi wa Azam FC wanaongoza timu kiungwana kama taasisi ya kiroho... siyo ya mpira.

Taasisi za kiroho hazihitaji ukorofi wa aina yoyote kwa sababu zinaongozwa na nguvu ya muumba, lakini siyo mpira.

Azam FC wanaendesha timu kiungwana kiasi kwamba hadi wachezaji wanaichukulia timu kama taasisi ya hisani badala ya ushindani.

Hebu dhania wachezaji wanachukua mikopo halafu hadi wanaondoka hawajalipa.

Wachezaji kama Salum Abubakary na Mudathir Yahya wameondoka Azam FC wakiacha madeni ambayo walikopa wakati wakiwa wachezaji...na hakuna anayejali.

Achana na hiyo, kuna hili suala la kuimarisha timu Kwa kuongeza wachezaji wapya na kuondoa ambao hawana msaada.

Nitaitilea Yanga kama mfano. Hivi karibuni ilitoka taarifa kwamba imeshitakiwa FIFA na kushindwa kesi na mchezaji wao wa zamani, Gael Bigirimana.

Mchezaji huyu alisajiliwa msimu wa 2022/23 lakini hakufikia matarajio, wakamuacha ili nafasi yake ichukukiwe na mchezaji mwingine atayeisaidia timu.

Wakafanya hivyo na timu yao ikaimarika. Kesi ilipoamuriwa kwamba Yanga wameshindwa, kiongozi mmoja mkuu wa klabu hiyo akasema, ‘timu ya mpira haigopi kesi za mikataba’.

Au rejea kisa cha Lazarus Kambole. Baada ya Yanga kumuona hana faida kwa timu yao, wakamchomoa kwenye mfumo wa usajili ili nafasi yake ichukuliwe na Tuisila Kisinda.

Mamlaka za mpira zikapinga zikisema sheria ya usajili hairuhusu mchezaji aliyesajiliwa msimu msimu huu, kutolewa kwenye mfumo msimu huo huo...badala yake anatakiwa kuhamishwa kutoka klabu hiyo kwenda klabu nyingine.

Ndipo ikaja taarifa kwamba Kambole kapelekwa Uganda.

Lakini kimsingi Kambole hakwenda Uganda, alikuwepo tu Dar Es Salaam. Kwanza alikuwa majeruhi, isingewezekana mchezaji majeruhi achukuliwe kwa mkopo na timu nyingine.

Hiki ndicho ambacho Azam FC wanakikosa pale Chamazi.

Msimu huu wakati wa dirisha la usajili, walitaka kumsajili Djuma Shaaban na kumtoa kipa Ali Ahamada.

Wakaongeza naye wamvunjie mkataba na kumlipa...akakataa, Azam FC wakaleta uungwana, wakamuachia Mungu.

Azam FC tayari wamenasa saini ya Djuma Shaaban lakini wameshindwa kumsajili.

Kwa hiyo wanakaa naye akifanya mazoezi na timu, wanamlipa mshahara na wamempangia hadi nyumba.

Lakini kwa kuwa Ali Ahamada alikataa kuondoka, basi wakashindwa kumsajili.

Kwa hiyo wanamlipa mshahara Djuma Shaaban, mchezaji ambaye hawasaidii kwa sasa. Na wanamlipa mshahara Ali Ahamada ambaye hawasaidii.

Hapo ndipo ule ukorofi ungehitajika kama wangekuwa nao.

Ali Ahamada angechomolewa kwenye usajili hata kama hataki ili Djuma Shaaban asajiliwe aisadie timu.

Halafu kama ataenda kushitaki, watajua cha kufanya baadaye lakini timu imepata faida.

Djuma Shaaban angeongeza kitu kikubwa sana kwa Azam FC. Uzoefu wake na maarifa yake vingekuwa na msaada mkubwa sana.

Upande ambao Djuma Shaaban angeenda kucheza, kwa sasa unamilikiwa na Lusajo Mwaikenda ambaye kiasili ni mlinzi wa kati.

Djuma angepatikana, Mwaikenda angerudi kati na kusaidia tatizo sugu pale kutokana na kukosekana mlinzi wa kati namba tano asilia.

Wanaocheza pale wote, Abdallah Kheri Sebo, Daniel Amoah, Malickou Ndoye na hata Edward Manyama, ni namba nne.

Lusajo peke yake ndiyo namba tano kwa hiyo Azam FC wamejikosesha kitu cha maana sana.

Kwa hiyo angeweza kucheza na mmojawapi katika hao wengine na kuimarisha safu ya ulinzi.

Lakini Ali Ahamada akakataa na viongozi wakakosa kale kaukorofi...klabu inakwama.

Hawa viongozi na huu uungwana wao ndiyo wanaikwamisha klabu.

Kwa misimu miwili mfululizo Azam FC imetolewa kwa mashindano ya Afrika katika uwanja wa nyumba huku wakikosa faida ya nyumbani.

Msimu uliopita dhidi ya Al Akhdar, kulikuwa na matukio matatu ambayo Azam FC kama timu ya nyumbani ilitakiwa kufaidika nayo kwa kupata penati.

Msimu huu dhidi ya Bahr Dar Kenema, Azam FC ingeweza kufaidika na matukio matano kama timu ya nyumbani, manne ya penati na moja la kadi nyekundu.

Mtu anaweza asielewe lakini sote tunajua nini maana ya kucheza nyumbani...nini maana ya faida ya nyumbani...nini maana ya home advantage.

Viongozi wenye ‘ukorofi’’ wa aina hii hawawezi kukubali kuona timu yao inatendewa vile katika uwanja wa nyumbani, mara mbili mfululizo.

Achana na hiyo, hebu angalia mechi zao pale Azam Complex. Mashabiki wanaoingia bure, lakini bado wanawazomea.

Halafu mchezo ujaoe, kiingilio tena bure. Unaona namna viongozi wa Azam FC wanavyopitiliza uungwana?

Uungwana wa namna hii hauisaidii timu badala yake unaikandamiza.

Wale mashabiki wanaokuja pale Azam Complex na kushangilia timu pinzani, wanawavunja moyo wachezaji wa Azam FC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live