Kocha Mkuu wa Azam, Dani Cadena amesema kikosi hicho hakitakuwa na mapumziko katika kipindi hichi cha michezo ya kimataifa isipokuwa ni kwa wale tu wachezaji ambao wameitwa kuziwakilisha timu zao za taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Cadena alisema kutakuwa na muda mrefu kwa wao kutocheza hivyo wameona ni vyema kutotoa ruhusa ya mapumziko kwa lengo la kurejesha morali ya timu yao baada ya kusuasua hivi karibuni.
"Ruhusa ambayo tumeitoa ni kwa wachezaji walioitwa timu za taifa tu ila wengine wote tutaendelea na mazoezi kwa lengo la kuhakikisha tunajiweka imara zaidi kutokana na michezo migumu iliyokuwa mbele yetu," alisema.
Aidha Cadena aliongeza katika kipindi hichi wako kwenye mchakato wa kutafuta angalau michezo hata miwili ya kirafiki ili waicheze akiamini ni njia nzuri itakayowarudisha katika ari wakati huu Ligi Kuu Bara imesimama.
"Tuko kwenye mazungumzo na baadhi ya timu na kama tutakubaliana basi tutacheza, itakuwa ni wakati mzuri pia kwa wachezaji walipo majeruhi kupata michezo hiyo itakayowaweka kwenye hali nzuri ya utimamu wa kimwili."
Mchezo wa mwisho kwa Azam ilikuwa ni Machi 13 wakati ilipochapwa bao 1-0 na Ihefu kwenye Uwanja wa Highland Estate na baada ya hapo itacheza na Mtibwa Sugar katika robo fainali ya Kombe la Azam (ASFC) kuanzia Aprili 1-6.
Sospeter Bajana na Abdul Suleiman 'Sopu' ni wachezaji wa Azam walioitwa katika kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kinachojiandaa na mchezo wa kufuzu AFCON mwakani dhidi ya Uganda, mechi itakayopigwa Machi 24 na 28.